KEMIKALI NA ASILIA
Ukiwa safarini ndani ya basi ni kawaida mkifika mahali
anapanda mtu ambaye anajitambulisha kwamba anafanya biashara ya madawa mbali
mbali. Ataanza kwa kuyaelezea magonjwa kwa jinsi anavyofahamu yeye na kisha
kuelezea dawa alizokuja nazo zinavyofanya kazi katika kutibu. Anapokuwa
anaendelea kuwavutia watu ili wanunue basi humo ndani ni lazima atasema kwamba
dawa zake hazina kemikali ila ni za asili. Hapo anakuwa anataka kuwaonesha
wateja wake tofauti ya dawa zake na hizi za kisasa akilaumu kemikali zilizomo
kwenye dawa za kisasa kwamba zinaweza kuleta madhara kwa binadamu. Huwa nacheka
kimoyomoyo pale wanapotaja orodha ya matatizo ambayo dawa zao zinatibu.
Matatizo hayo huwa kama vile: kuumwa jino, kuumwa na nyuki ama nge, kunuka
mdomo, kuwashwa, kuacha pombe, kuacha sigara, kutokwa na uchafu ukeni, kunuka
nguo za ndani, kunuka kwapa, kunuka miguu na kadharika. Dawa ambazo wanakuja
nazo huwa ni pamoja na dawa za meno, sabuni, lotion vyenye picha za majani kama
vile alovera ama mwarobaini, na nyingine huwa zimo kwenye vichupa vyenye
maandishi ya kichina.
Inaonekana soko la hawa watu limelalia kwenye kile
wanachodai dawa zile hazina kemikali ila ni za asili ili mteja wao aone sababu
kwa nini asiende kwenye duka la dawa za binadamu na anunue zile. Kama ulisoma
hapa nchini kwetu unaweza kuwa ulipita sekondari na ukafundishwa somo la kemia
ila usijue maana ya kemikali kwa sababu kitabu wanachotumia kidato cha kwanza
Tanzania hakijatoa maana ya hili neno. Kwa urahisi wake tu na kisayansi
kemikali ni kitu chochote kile; kuanzia maji tunayotumia, vyakula tunavyokula,
miili yetu hii yenyewe imeundwa na kemikali, miti, majani, maua, miziz na
matunda ambamo dawa za “asili” zinatoka nayo ni kemikali, kwenye ubongo wetu
kuna kemikali zinazotufanya tujisikie furaha ama huzuni, tumboni mwetu kuna
kemikali zinazotusaidia kumeng’enya chakula, mate na machozi yetu nayo ni
kemikali, chumvi, sukari na vyote unavyovijua ni kemikali. Tunaweza kuishi bila
kemikali kweli? Labda huwa wanamaamisha wanavyoviuza havijapitia kiwandani
katika utengenezaji ukilinganisha na hizi dawa za kisasa! Ndiyo, miti shamba
huwa haijapita kiwandani ila zile sabuni na dawa za meno vyenye picha za majani
majani huwa nazo zimepita viwandani, naamini wanatumia mwanya wa wateja wao kutokujua
neno kemikali na kujipatia faida pasi hata na kulipa kodi.
Watu hawa wanaouza hizi dawa wanaonekana hawana ujuzi na
wanachokifanya ila tu wanajitafutia kipato. Kinachonishangaza ni kuna wengine
ambao wana elimu ya juu katika kada ya afya nao wanajihusisha na hii biashara.
Wapo wanaouza dawa za “asili” za kupunguza unene zisizo na “kemikali”
wakiwaambia wateja wao kwamba hakuna haja ya mazoezi wala kupunguza na kuchagua
vyakula. Mmoja alinikalisha chini kipindi fulani akinielezea kuhusu tezi dume
(kwa usahihi kabisa) kisha akaomba aniuzie majani ya chai yatakayonizuia
nisipate tezi dume(wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 22)
Kufikiri kwamba kitu kikiwa ni cha asili basi ni salama na
hakina madhara ni kupotea sana. Kuna mimea yenye sumu ambayo yaweza kukuletea
matatizo. Sumu hizi zinaweza zisiue papo hapo ila zikaleta madhara makubwa
baadae kama vile matatizo ya figo ama ini. Ni kweli kwamba dawa za kisasa nazo
zaweza kukuletea matatizo ambayo hayakudhamiriwa(side effects) lakini hiyo
hutokea pia kwa dawa za asili. Lakini kuna tofauti, dawa za kisasa zimepitia
majaribio kabla ya kuruhusiwa na nyingine zinaafamika madhara yake na unaweza
kupewa ushauri kabla ya kuzitumia; dawa za kisasa hufahamika kiasi ambacho mtu
hutakiwa kupewa kwa ugonjwa fulani hivyo kupunguza uwezekano wa kuzidisha kiasi
ukilinganisha na zile za asili ambazo maandalizi yake(kupondaponda, kuchemsha,
kuchoma, n.k) hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine; dawa za kisasa
zinaonesha nini kilichomo kwenye dawa hiyo tofauti na zile za asili ambazo
unakuwa hujui nini kilichomo ndani bali unaambiwa tu ni dawa ya kutibu kitu fulani.
Maandalizi ya dawa za kisasa yanaeleweka na yanafuata taratibu kama vile
kuondoa vitu visivyofaa ili vibaki vile byenye kutibu na visivyo na madhara kwa
binadamu, maandalizi ya dawa za asili hayana teknolojia ya kuchambua baadhi ya
vitu visivyofaa mfano madini ya zebaki na hivyo dawa zinakuja zimechanganyikana
na vitu vinavyoweza kuleta madhara kiafya.
Ni kweli kwamba changamoto zilizopo kwenye huduma za afya
hii ya kisasa, gharama na kushindwa kutibu baadhi ya magonjwa kikamilifu kunawafanya
watu waangalie njia nyingine. Njia mojawapo ni hizi za asili. Binafsi nimewaona
watu wenye uwezo wa kuchagua wakiachana na hizi dawa za kisasa kwa kuambiwa
zile za asili hazina madhara ukilinganisha na za kisasa kwa sababu tu hizo ni
kemikali. Tufahamu tu basi asilia haimaanishi salama na huenda ikawa na madhara
Zaidi.
"Asili haidhuru" huu nao ni msemo wa wahenga
ReplyDeleteHehehehe,
DeleteI see
Well said brother.Mamlaka za udhibiti (TFDA) waongeze kasi kwenye udhibiti wa advertisement and promotion ya hizi dawa hasa kwenye mitandao ya kijamii na sisi huku tuendelee kutoa elimu kuepusha madhara zaidi
ReplyDeleteYeah ni kweli
DeleteAsante Sana mkuu,
ReplyDeleteUnaongea kitaalamu.
Pamoja sana mkuu
Delete