Saturday, 1 October 2016

KEMIKALI NA ASILIA


KEMIKALI NA ASILIA
Ukiwa safarini ndani ya basi ni kawaida mkifika mahali anapanda mtu ambaye anajitambulisha kwamba anafanya biashara ya madawa mbali mbali. Ataanza kwa kuyaelezea magonjwa kwa jinsi anavyofahamu yeye na kisha kuelezea dawa alizokuja nazo zinavyofanya kazi katika kutibu. Anapokuwa anaendelea kuwavutia watu ili wanunue basi humo ndani ni lazima atasema kwamba dawa zake hazina kemikali ila ni za asili. Hapo anakuwa anataka kuwaonesha wateja wake tofauti ya dawa zake na hizi za kisasa akilaumu kemikali zilizomo kwenye dawa za kisasa kwamba zinaweza kuleta madhara kwa binadamu. Huwa nacheka kimoyomoyo pale wanapotaja orodha ya matatizo ambayo dawa zao zinatibu. Matatizo hayo huwa kama vile: kuumwa jino, kuumwa na nyuki ama nge, kunuka mdomo, kuwashwa, kuacha pombe, kuacha sigara, kutokwa na uchafu ukeni, kunuka nguo za ndani, kunuka kwapa, kunuka miguu na kadharika. Dawa ambazo wanakuja nazo huwa ni pamoja na dawa za meno, sabuni, lotion vyenye picha za majani kama vile alovera ama mwarobaini, na nyingine huwa zimo kwenye vichupa vyenye maandishi ya kichina.
 Image result for natural vs chemical
Inaonekana soko la hawa watu limelalia kwenye kile wanachodai dawa zile hazina kemikali ila ni za asili ili mteja wao aone sababu kwa nini asiende kwenye duka la dawa za binadamu na anunue zile. Kama ulisoma hapa nchini kwetu unaweza kuwa ulipita sekondari na ukafundishwa somo la kemia ila usijue maana ya kemikali kwa sababu kitabu wanachotumia kidato cha kwanza Tanzania hakijatoa maana ya hili neno. Kwa urahisi wake tu na kisayansi kemikali ni kitu chochote kile; kuanzia maji tunayotumia, vyakula tunavyokula, miili yetu hii yenyewe imeundwa na kemikali, miti, majani, maua, miziz na matunda ambamo dawa za “asili” zinatoka nayo ni kemikali, kwenye ubongo wetu kuna kemikali zinazotufanya tujisikie furaha ama huzuni, tumboni mwetu kuna kemikali zinazotusaidia kumeng’enya chakula, mate na machozi yetu nayo ni kemikali, chumvi, sukari na vyote unavyovijua ni kemikali. Tunaweza kuishi bila kemikali kweli? Labda huwa wanamaamisha wanavyoviuza havijapitia kiwandani katika utengenezaji ukilinganisha na hizi dawa za kisasa! Ndiyo, miti shamba huwa haijapita kiwandani ila zile sabuni na dawa za meno vyenye picha za majani majani huwa nazo zimepita viwandani, naamini wanatumia mwanya wa wateja wao kutokujua neno kemikali na kujipatia faida pasi hata na kulipa kodi.

Watu hawa wanaouza hizi dawa wanaonekana hawana ujuzi na wanachokifanya ila tu wanajitafutia kipato. Kinachonishangaza ni kuna wengine ambao wana elimu ya juu katika kada ya afya nao wanajihusisha na hii biashara. Wapo wanaouza dawa za “asili” za kupunguza unene zisizo na “kemikali” wakiwaambia wateja wao kwamba hakuna haja ya mazoezi wala kupunguza na kuchagua vyakula. Mmoja alinikalisha chini kipindi fulani akinielezea kuhusu tezi dume (kwa usahihi kabisa) kisha akaomba aniuzie majani ya chai yatakayonizuia nisipate tezi dume(wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 22)

Kufikiri kwamba kitu kikiwa ni cha asili basi ni salama na hakina madhara ni kupotea sana. Kuna mimea yenye sumu ambayo yaweza kukuletea matatizo. Sumu hizi zinaweza zisiue papo hapo ila zikaleta madhara makubwa baadae kama vile matatizo ya figo ama ini. Ni kweli kwamba dawa za kisasa nazo zaweza kukuletea matatizo ambayo hayakudhamiriwa(side effects) lakini hiyo hutokea pia kwa dawa za asili. Lakini kuna tofauti, dawa za kisasa zimepitia majaribio kabla ya kuruhusiwa na nyingine zinaafamika madhara yake na unaweza kupewa ushauri kabla ya kuzitumia; dawa za kisasa hufahamika kiasi ambacho mtu hutakiwa kupewa kwa ugonjwa fulani hivyo kupunguza uwezekano wa kuzidisha kiasi ukilinganisha na zile za asili ambazo maandalizi yake(kupondaponda, kuchemsha, kuchoma, n.k) hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine; dawa za kisasa zinaonesha nini kilichomo kwenye dawa hiyo tofauti na zile za asili ambazo unakuwa hujui nini kilichomo ndani bali unaambiwa tu ni dawa ya kutibu kitu fulani. Maandalizi ya dawa za kisasa yanaeleweka na yanafuata taratibu kama vile kuondoa vitu visivyofaa ili vibaki vile byenye kutibu na visivyo na madhara kwa binadamu, maandalizi ya dawa za asili hayana teknolojia ya kuchambua baadhi ya vitu visivyofaa mfano madini ya zebaki na hivyo dawa zinakuja zimechanganyikana na vitu vinavyoweza kuleta madhara kiafya.

Ni kweli kwamba changamoto zilizopo kwenye huduma za afya hii ya kisasa, gharama na kushindwa kutibu baadhi ya magonjwa kikamilifu kunawafanya watu waangalie njia nyingine. Njia mojawapo ni hizi za asili. Binafsi nimewaona watu wenye uwezo wa kuchagua wakiachana na hizi dawa za kisasa kwa kuambiwa zile za asili hazina madhara ukilinganisha na za kisasa kwa sababu tu hizo ni kemikali. Tufahamu tu basi asilia haimaanishi salama na huenda ikawa na madhara Zaidi.

6 comments:

  1. "Asili haidhuru" huu nao ni msemo wa wahenga

    ReplyDelete
  2. Well said brother.Mamlaka za udhibiti (TFDA) waongeze kasi kwenye udhibiti wa advertisement and promotion ya hizi dawa hasa kwenye mitandao ya kijamii na sisi huku tuendelee kutoa elimu kuepusha madhara zaidi

    ReplyDelete
  3. Asante Sana mkuu,
    Unaongea kitaalamu.

    ReplyDelete