Sunday, 18 December 2016

TUJENGE UTAMADUNI WA KUPENDA KUSOMA



Marehemu Langa aliwahi kuimba kwamba “ukitaka kumficha mwafrika weka ujumbe kwenye vitabu”. Langa alimaanisha kuwa sisi hatuna tamaduni ya kupenda kupekua-pekua vitabu. Hili siyo jambo jema lakini kizuri Zaidi ni kwamba hii tabia si ya kurisi kama tulivyorisi rangi zetu bali tunaweza kubadilika na kuutengeneza utamaduni huu miongoni mwetu baada tu ya kutambua umuhimu wake na kutengeneza mifumo ya kuwezesha hilo kutokea.
 Image result for reading culture
Binafsi naamini kupitia kusoma ni njia kuu ya kujitoa kwenye matatizo tuliyonayo. Ukweli wa hili unajidhihirisha hata kwenye historia. Kipindi mtu mweusi alipoishi kama mtumwa nchini Marekani ni kipindi ambacho pia hakuruhusiwa kujua kusoma wala kuandika, sheria zao zilikataza kabisa mtu mweusi kupelekwa shule na bwana wake. Walijua kabisa mtu yule alikuwa ana akili na kama angejua kusoma basi hiyo ingekuwa kama tochi yake kuona yale asiyotakiwa kuyaona na huo ungekuwa mwisho wa unyonyaji na ukandamizaji ulioendelea. Hata vuguvugu la kutafuta haki za watu weusi lililetwa na wale wachache ambao kwa bahati ya mtende waliweza kujua kusoma. Huko Afrika ya Kusini pia makaburu walibana elimu kwa watu weusi ukilinganisha na wao wenyewe, hata Mandela mwenyewe alipata elimu kwa sababu baba yake alikuwa mshauri wa chifu na alipofariki alilelewa na chifu. Hata hapa kwetu wakoloni hawakutoa elimu kwa faida yetu bali kwa faida zao pale ilipowabidi kama vile kusomesha watoto wa machifu ili waelewane na machifu.

Mfano mkubwa kabisa katika kuonesha kusoma kunaweza kubadilisha maisha ya mtu ni wa kijana mmalawi aitwaye William Kamkwamba. Kamkwamba alizaliwa kwenye familia masikini huko kijijini kwao Masitala karibu na jiji la Kasungu. Alipokuwa anaingia kuanza elimu yake ya sekondari, Malawi ilikuwa imekumbwa na mafuriko yaliyoambatana na njaa kitu ambacho kilimfanya baba yake ashindwe kumlipia ada ya shule. Kamkwamba alibaki nyumbani ila hakukaa tu bali alipenda kwenda maktaba kujisomea ili angalau awe sambamba na wenzake pindi ada itakapopatikana na akarudi shule. Alisoma vitabu mbalimbali ila kilichobadilisha maisha yake anasema kiliitwa Explaining Physics ambacho kilieleza jinsi kata upepo inavyofanya kazi na kutengeneza umeme. Kwa kutumia kitabu hicho aliweza kutengeneza kata upepo kwa kuunga-unga kutoka kwenye vitu alivyookota jalalani likatoa umeme akawasha taa kwao na akatumia kuchaji simu za wanakijiji. Aliwahi pia kutengeneza bayogesi na pampu ya kuvuta maji kutoka kisimani japo havikufanikiwa kutokana na kukosa vifaa. Cha ajabu shule za serikali za Malawi zilipoombwa kumuingiza aendelee na elimu yake zilisema alikuwa ana umri mkubwa, na hata serikali ya Malawi haikujua wala haikumsaidia chochote katika kukuza kipaji chake; na hata alipokutana na raisi Bingu Wa Mutharika alipokuwa amealikwa kwenye mkutano mmoja huko Afrika Kusini ndio ilikuwa mara ya kwanza rais anamuona William na kwa mara ya kwanza anasikia habari zake. William alipata scholarship kwenye shule ya international na baadae akaenda kusoma African Leadership Academy kabla ya kwenda kusoma uinjinia chuo kikuu cha Dartmouth nchini Marekani.

Wengi mara ya mwisho kusoma huwa ni pale tukiwa shuleni na mara nyingi tunasoma field zinazotuhusu tu. Ni vigumu kumkuta mwanafunzi wa udaktari labda anasoma kitabu cha historia, filosofia ama astrofizikia. Lakini hatuwezi kuzungumza kuwa hatuna utamaduni wa kupenda kusoma bila kugusa upande wa pili kwamba hatuna pia utamaduni wa kuuandikia umma (tunao wataalamu wanaoandika sana machapisho ya tafiti ila ni katika kada zao za elimu, tofauti na kuuandikia umma). Nikitembelea maduka ya vitabu, vitabu vingi ninavyoviona huwa ni vya kujifunzia mashuleni  na vingine huwa vimetoka nje ya nchi ambavyo huwa vinawaelekeza watu jinsi ya kupata mafanikio maishani. Vilivyoandikwa na watanzania wenzetu huwa ni kimoja kimoja ukiachilia mbali vijitabu vyenye stori za watu wanaodai wamewahi kupelekwa kuzimu na mambo mengine ya uchawi ambayo huwa ni uwongo tu. Huwa najiuliza kama tunataka kujifunza kuhusu kufanikiwa katika mazingira ya kitanzania kwanini watu kama akina Mo Dewji, Mengi ama Bakhresa wasituandikie tuyasome mawazo yao. Kwanini wazee waliopata bahati ya kusoma enzi za mwalimu wasituandikie mawazo yao kuhusu hali ya nchi inavyokwenda. Kwanini wanasayansi wachache tulio nao wasituandikie kuhusu maendeleo ya sayansi ama nini kifanyike kuhusu sayansi nchini kwetu. Watu waliofanikiwa kwenye sekta zao kama akina Platinums na Samata waweza kuongea na wengine wanaotaka kuwa kama wao kupitia vitabu na sio kwa kuwafollow tu kwenye instagram.

Ni dhahir pia hatujaweka mazingira mazuri yenye kuamsha utamaduni wa kupenda kusoma. Tukijenga nyumba zetu nzuri za gharama tunaweka sebure nzuri ili wageni watupe sifa ila tunasahau kuweka maktaba na kuzijaza vitabu. Kama kuna kitu sijawahi kusikia serikali hata ikikiongelea huwa ni maktaba zake, mara ya mwisho naingia maktaba ya mkoa wa mwanza ilikuwa mwaka 2011  ila vitabu vyake vilikuwa ni vya muda mrefu vilivyochoka na kulikuwa na kiingilio. Wengi waliokuwa mule walikuwa ni wanafunzi wa sekondari waliokwenda pale ili kupata utulivu wa kujisomea mambo yao ya shuleni. Vitabu vingi huwa tunapewa kama misaada japo tuna watu wenye uwezo wa kulipia watu mamilioni ya pesa waangalie mpira bure zaidi ya mara moja. Kila mtaa wetu una banda la kuangalizia mpira unaorushwa kutoka upande mwingine wa dunia na tunalipia ila hatuwezi kuweka hata ka maktaba cha watoto wadogo. Mashuleni kwetu si tu kwamba watoto wanakosa vitabu vya kujifunzia bali wakati mwingine hata mwalimu anakosa kitabu cha kufundishia

Mwaka 2013 nilipoona kuna ugumu wa kupata vitabu hapa nchini nilisaidiwa na rafiki yangu kuagiza kifaa kwa jili ya kusomea kiitwacho kindle. Kilikuja bila kava na nikaamua kulitafuta kava lake kwenye maduka ya jiji letu kuu la Dar es salaam. Nilishangazwa pale nilipoona kuwa maduka yoote niliyotembelea yakiwemo ya kariakoo, mlimani city, posta na kwingine hayakuifahamu kindle na hawajawahi hata kuisikia. Mmoja kati ya wauzaji aliniuliza “unasema unatafuta kinu?”. Ila jibu la kwanini kifaa hiki hakikujulikana kwenye maduka haya miaka takribani 6 baada ya kuanza kutolewa na kampini la Amazon ni kwa sababu hakina kazi nyingine zaidi ya kusomea tu. Simu za gharama zikitoka huwa zinapatikana nchini ndani ya mwezi huohuo ziliotolewa. Tunaishi kwenye dunia ya kiteknolojia zaidi ya wakati wowote duniani, na kitu muhimu ni nini kimo ndani ya vichwa vyetu. Tutaweza kuendana na dunia hii kwa kupenda kuongeza ujuzi na njia ya kufanya hilo ni kwa kusoma. Tukuze utamaduni wa kupenda kusoma.

0 comments:

Post a Comment