Sunday, 11 September 2016

MATUMIZI MABAYA YA MAABARA ZA BINAFSI

MATUMIZI MABAYA YA MAABARA ZA BINAFSI

Miaka 10 iliyopita nilikua nasumbuliwa na tumbo na kama ilivyo kawaida yetu badala ya kwenda hospitalini kumuona daktari, babu yangu alinipa pesa akinielekeza nikapime choo na damu kwenye ki-maabara kimojawapo hapo mjini. nilipofika pale nilieleza nimekuja kupima choo na damu, hakuna alievutiwa hata na kujua kwa nini napima. Sikumbuki vizuri iligharimu kiasi gani cha fedha ila ninachokumbuka ni yule aliyenitoa damu hakuvaa koti jeupe na baada ya kuingiza sindano aliniuliza “ulisema unaitwa nani vile?” nikajibu kwa kigugumizi wakati yeye na mwenzie aliyekua pembeni wakikenua meno. Hawakuwa na chembe ya maadili ya kazi na heshima kwa mgonjwa, sidhani kama walikuwa wamesomea kazi ile. Baada ya kutoa damu na kuwapa choo kwenye kasha la kiberiti walimpa mtu mwingine aliyekua amekaa pembeni akichunguza vinyesi na damu kwenye darubini ndogo iliyotumia taa ya umeme, baada ya hapo nilikaa kwenye foleni pamoja na wagonjwa wengine tukisubiri kuingia kwenye chumba kilichoandikwa “chumba cha daktari”. Ilipofika zamu yangu niliingia kwenye kile chumba nikamkuta yule aliyekuwa akichunguza vinyesi na damu kwenye darubini hapo mwanzo. “unaitwa nani?” aliniuliza, baada ya kumwambia akatafuta kikaratasi chenye jina langu akakifungua akaniambia “una amiba, nitakuandikia dawa ukanunue, alafu punguza kula kachumbari ndio zinasababisha uumwe.” Nilipokwenda kwenye duka la dawa baridi nikawapa kile kikaratasi walinipa dawa aina ya Mebendazole. Nilikunywa ila sikuona nafuu na baada ya siku kadhaa tumbo lilitulia lenyewe ila hali hii ilijirudia mara kwa mara na kila nilipoenda tena niliambiwa ni amiba ambayo baadae walisema itakua ni amiba sugu na muda mwingine walisema nina “fangasi tumboni”(hata leo sijui walimaanisha nini) na wakasema watanifanyia culture*.

Nilipokwenda hospitalini baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu nilionana na daktari, akanisikiliza, nikamuelezea dalili nilizokua nazo ikiwemo: tumbo kuuma sana wakati nikiwa na njaa na kutulia punde tu ninapokula kitu, kuamshwa usiku wa manane na maumivu ya tumbo na kutapika. Daktari alisema anahisi ni vidonda vya tumbo na kuniambia nifanye vipimo, baada ya vipimo alisema nilikua nasumbuliwa na vidonda vya tumbo kama alivyo waza na alinipa dawa ambazo baada ya kutumia tumbo lilitulia. Nilijifunza tofauti ya sehemu hizi mbili na ninajua wengine wanateseka kama nilivyoteseka mimi na leo nachukua nafasi hii tuelimishane kuhusu utumiaji mbovu wa hizi maabara ambazo zinafunguliwa kwa wingi siku hizi na zinafanya kazi bila kufuata taratibu.

Imekua kawaida miongoni mwetu mtu akijisikia ana homa basi anahisi anajua anaumwa nini na anachotaka kufanya ni kupata uhakika wa anachohisi, atasema “hii itakua malaria, ngoja nikapime malaria” akienda maabara nao wanamwambia “una malaria tatu” nae anaridhika na kusema “nilijua tu, sema hii ni ndogo sana haitanisumbua sana” alafu wale wa maabara wanamuuliza “ huwa unatumia dawa gani ya malaria?” naye anajibu “fansidar” basi anaenda kununua fansidar anabugia. Hayo yamekwishawahi kunitokea hata mimi. Nachotaka kukwambia ni kwamba tuna bahati sana. Bwana mmoja wa karibu yangu aliyewahi kufanya kazi kwenye moja ya maabara hizi aliniambia kila aliepima malaria majibu yalitoka kwamba anayo na alipouliza kwa nini wanafanya hivyo aliambiwa wateja wanapenda kusikia hivyo na ukiwaambia  hawana wataenda sehemu nyingine na kule wakiambiwa wanayo wewe utakosa soko, sababu nyingine ilikua ni kukosa kemikali za kutumia ili kuona vimelea. Hata hivyo, kukutwa na vimelea vya malaria kwenye damu kwa sisi tunaoishi haya maeneo yenye malaria haimaanishi tunaumwa malaria. Pia, hivi karibuni utafiti katika chuo kikuu cha Sokoine umeonesha kwamba homa nyingine hapa nchini husababishwa na ugonjwa wa Leptospirosis, hii inamaanisha kuna sababu nyingi za homa. Kwa kuongezea, nimesema tuna bahati kwa sababu dawa tunazopewa huko huenda zisiwe zile zilizosisitizwa na wizara ya afya kutokana na utafiti, huyu mtu aliekunywa Fansidar kwa mfano huenda akaingia gharama kubwa Zaidi na hata kugharimu maisha yake pale atakapolazimika kulazwa baada ya kupata Malaria kali, ama kufeli kwa figo zake kama tatizo linaloweza kuambatana na malaria kali.

Akiwa kama wakili wa afya njema, Daktari amebobea katika kutambua mgonjwa anasumbuliwa na ugonjwa gani kutokana na dalili alizonazo. Ana ujuzi mpana juu ya jinsi magonjwa mbali mbali yanavyojionesha alioupata kwa miaka mingi shuleni. Amejifunza pia jinsi ya kuweza kuhakiki kile anachofikiria kinaweza kikawa ndicho kinachomsumbua mgonjwa, hapa huweza kuagiza vipimo mbali mbali kama vya damu, choo, mkojo, picha za x-ray na kadhalika; hapa ndipo kazi ya mtaalamu wa maabara inakuja, yeye amebobea katika kuweza kuvitambua vitu mbali mbali vilivyomo kwenye damu, choo, mkojo, na vingine kutoka kwa mgonjwa (vitu hivi hata daktari hawezi kuvifanya kwa ufanisi kama mtaalamu wa maabara). Kwa kua kuna vitu vingi sana vya kuangalia kwenye damu, mkojo ama choo cha mgonjwa, basi daktari huagiza vitu kadhaa ambavyo vitamsaidia kujua mgonjwa anaumwa nini kutokana na dalili zake. Daktari pia amejifunza jinsi ya kuyatibu magonjwa pale anapokua ameyafahamu aidha kutokana na vipimo ama bila vipimo. Kwa kuongezea, daktari pia amejifunza kumfuatilia mgonjwa baada ya kumpa matibabu kuona maendeleo yake na kumpa ushauri pale unapohitajika.

Wanaomiliki maabara binafsi wanasaidia kwa kiasi kikubwa, na ninatambua mchango wao katika kuboresha afya za jamii. Lakini natambua pia ni wanafanya biashara na kama tunavyojua biashara ni faida. Ni bora basi kuwaelimisha wateja wao ili wakafanya maamuzi wakiwa na ujuzi. Utaratibu sahihi ni kuanzia kuonana na daktari kwanza akusikilize, halafu yeye anaweza amua ufanye vipimo kwanza ama akupe dawa moja kwa moja, hiki ndicho alichotumia kodi yako kukisomea. Pale inapoonekana kipimo fulani hakipatikani katika maabara ya hapo unaweza enda kwenye maabara sasa kufanya kipimo hicho kwa maelekezo kutoka kwa daktari. Baadae daktari atakupa dawa sahihi ya kutumia ambayo inasisitizwa na wizara ya afya kwa wakati huo. Kama ni ugonjwa mkubwa ambao bado upo katika hatua za mwanzo, daktari ana uwezo wa kuutambua kuliko mtu ambae sio daktari, hii itasaidia kuuwahi katika matibabu kabla haujafika mbali. Kujipa majukumu ya daktari ama kuwapa majukumu hayo wataalamu wa maabara ni sawa na kujijengea nyumba wakati ukijua wewe si fundi muashi, itakuangukia.













*culture ni uoteshaji wa vimelea kwenye mazingira ambayo ni pendelevu kwa vimelea husika kwa lengo la kutaka kuvifahamu. Kwa mfano wanataka kujua kama kwenye damu yako kuna aina fulani ya vimelea basi wanachukua damu yako na kuiweka kwenye mazingira ambayo vimelea vile vingeota kama kweli vipo kwenye damu yako.

9 comments:

  1. Njema sana Dr.this is good staff

    ReplyDelete
  2. Hii imekuwa desturi yetu kwa miaka mingi. Kwa namna moja au nyingine magonjwa mengi ambayo amefika hatua mbaya yangeweza kuzuilika kama tungekuwa na utaratibu wa kwenda hospitali.
    Mbali na hayo katika mazungumzo ya hapa na pale na baadhi ya watu nimepata sababu nyingine zinazowafanya watu kupenda kutumia maabara zetu za mitaani kama mbadala wa hospitali,ni kama moja msongamano wa watu hospitali ambayo hufanya watu kutumia siku nzima
    Pili kuhisi wanachoumwa ni kidogo tu hakiihitaji sana kumuona daktari na tatu ni kutopata ushirikiano mzuri kutoka kwa watoa huduma za afya hospitalini. Kuboresha huduma za afya na kutoa elimu kwa jamii(kama Joseph Julius )itasaidia sana kupunguza tatizo hili

    ReplyDelete