MATUMIZI MABAYA YA
MAABARA ZA BINAFSI
Miaka 10 iliyopita nilikua nasumbuliwa na tumbo na kama
ilivyo kawaida yetu badala ya kwenda hospitalini kumuona daktari, babu yangu
alinipa pesa akinielekeza nikapime choo na damu kwenye ki-maabara kimojawapo
hapo mjini. nilipofika pale nilieleza nimekuja kupima choo na damu, hakuna
alievutiwa hata na kujua kwa nini napima. Sikumbuki vizuri iligharimu kiasi
gani cha fedha ila ninachokumbuka ni yule aliyenitoa damu hakuvaa koti jeupe na
baada ya kuingiza sindano aliniuliza “ulisema unaitwa nani vile?” nikajibu kwa
kigugumizi wakati yeye na mwenzie aliyekua pembeni wakikenua meno. Hawakuwa na
chembe ya maadili ya kazi na heshima kwa mgonjwa, sidhani kama walikuwa
wamesomea kazi ile. Baada ya kutoa damu na kuwapa choo kwenye kasha la kiberiti
walimpa mtu mwingine aliyekua amekaa pembeni akichunguza vinyesi na damu kwenye
darubini ndogo iliyotumia taa ya umeme, baada ya hapo nilikaa kwenye foleni
pamoja na wagonjwa wengine tukisubiri kuingia kwenye chumba kilichoandikwa “chumba
cha daktari”. Ilipofika zamu yangu niliingia kwenye kile chumba nikamkuta yule
aliyekuwa akichunguza vinyesi na damu kwenye darubini hapo mwanzo. “unaitwa
nani?” aliniuliza, baada ya kumwambia akatafuta kikaratasi chenye jina langu
akakifungua akaniambia “una amiba, nitakuandikia dawa ukanunue, alafu punguza
kula kachumbari ndio zinasababisha uumwe.” Nilipokwenda kwenye duka la dawa
baridi nikawapa kile kikaratasi walinipa dawa aina ya Mebendazole. Nilikunywa ila sikuona nafuu na baada ya siku kadhaa
tumbo lilitulia lenyewe ila hali hii ilijirudia mara kwa mara na kila
nilipoenda tena niliambiwa ni amiba ambayo baadae walisema itakua ni amiba sugu
na muda mwingine walisema nina “fangasi tumboni”(hata leo sijui walimaanisha
nini) na wakasema watanifanyia culture*.
Nilipokwenda hospitalini baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu
nilionana na daktari, akanisikiliza, nikamuelezea dalili nilizokua nazo
ikiwemo: tumbo kuuma sana wakati nikiwa na njaa na kutulia punde tu ninapokula
kitu, kuamshwa usiku wa manane na maumivu ya tumbo na kutapika. Daktari alisema
anahisi ni vidonda vya tumbo na kuniambia nifanye vipimo, baada ya vipimo
alisema nilikua nasumbuliwa na vidonda vya tumbo kama alivyo waza na alinipa
dawa ambazo baada ya kutumia tumbo lilitulia. Nilijifunza tofauti ya sehemu
hizi mbili na ninajua wengine wanateseka kama nilivyoteseka mimi na leo
nachukua nafasi hii tuelimishane kuhusu utumiaji mbovu wa hizi maabara ambazo
zinafunguliwa kwa wingi siku hizi na zinafanya kazi bila kufuata taratibu.
Imekua kawaida miongoni mwetu mtu akijisikia ana homa basi
anahisi anajua anaumwa nini na anachotaka kufanya ni kupata uhakika wa
anachohisi, atasema “hii itakua malaria, ngoja nikapime malaria” akienda
maabara nao wanamwambia “una malaria tatu” nae anaridhika na kusema “nilijua
tu, sema hii ni ndogo sana haitanisumbua sana” alafu wale wa maabara
wanamuuliza “ huwa unatumia dawa gani ya malaria?” naye anajibu “fansidar” basi
anaenda kununua fansidar anabugia. Hayo yamekwishawahi kunitokea hata mimi.
Nachotaka kukwambia ni kwamba tuna bahati sana. Bwana mmoja wa karibu yangu
aliyewahi kufanya kazi kwenye moja ya maabara hizi aliniambia kila aliepima
malaria majibu yalitoka kwamba anayo na alipouliza kwa nini wanafanya hivyo
aliambiwa wateja wanapenda kusikia hivyo na ukiwaambia hawana wataenda sehemu nyingine na kule
wakiambiwa wanayo wewe utakosa soko, sababu nyingine ilikua ni kukosa kemikali
za kutumia ili kuona vimelea. Hata hivyo, kukutwa na vimelea vya malaria kwenye
damu kwa sisi tunaoishi haya maeneo yenye malaria haimaanishi tunaumwa malaria.
Pia, hivi karibuni utafiti katika chuo kikuu cha Sokoine umeonesha kwamba homa
nyingine hapa nchini husababishwa na ugonjwa wa Leptospirosis, hii inamaanisha kuna sababu nyingi za homa. Kwa
kuongezea, nimesema tuna bahati kwa sababu dawa tunazopewa huko huenda zisiwe
zile zilizosisitizwa na wizara ya afya kutokana na utafiti, huyu mtu aliekunywa
Fansidar kwa mfano huenda akaingia gharama kubwa Zaidi na hata kugharimu maisha
yake pale atakapolazimika kulazwa baada ya kupata Malaria kali, ama kufeli kwa
figo zake kama tatizo linaloweza kuambatana na malaria kali.
Akiwa kama wakili wa afya njema, Daktari amebobea katika
kutambua mgonjwa anasumbuliwa na ugonjwa gani kutokana na dalili alizonazo. Ana
ujuzi mpana juu ya jinsi magonjwa mbali mbali yanavyojionesha alioupata kwa
miaka mingi shuleni. Amejifunza pia jinsi ya kuweza kuhakiki kile anachofikiria
kinaweza kikawa ndicho kinachomsumbua mgonjwa, hapa huweza kuagiza vipimo mbali
mbali kama vya damu, choo, mkojo, picha za x-ray na kadhalika; hapa ndipo kazi
ya mtaalamu wa maabara inakuja, yeye amebobea katika kuweza kuvitambua vitu
mbali mbali vilivyomo kwenye damu, choo, mkojo, na vingine kutoka kwa mgonjwa
(vitu hivi hata daktari hawezi kuvifanya kwa ufanisi kama mtaalamu wa maabara).
Kwa kua kuna vitu vingi sana vya kuangalia kwenye damu, mkojo ama choo cha
mgonjwa, basi daktari huagiza vitu kadhaa ambavyo vitamsaidia kujua mgonjwa
anaumwa nini kutokana na dalili zake. Daktari pia amejifunza jinsi ya kuyatibu
magonjwa pale anapokua ameyafahamu aidha kutokana na vipimo ama bila vipimo.
Kwa kuongezea, daktari pia amejifunza kumfuatilia mgonjwa baada ya kumpa
matibabu kuona maendeleo yake na kumpa ushauri pale unapohitajika.
Wanaomiliki maabara binafsi wanasaidia kwa kiasi kikubwa, na
ninatambua mchango wao katika kuboresha afya za jamii. Lakini natambua pia ni wanafanya
biashara na kama tunavyojua biashara ni faida. Ni bora basi kuwaelimisha wateja
wao ili wakafanya maamuzi wakiwa na ujuzi. Utaratibu sahihi ni kuanzia kuonana
na daktari kwanza akusikilize, halafu yeye anaweza amua ufanye vipimo kwanza
ama akupe dawa moja kwa moja, hiki ndicho alichotumia kodi yako kukisomea. Pale
inapoonekana kipimo fulani hakipatikani katika maabara ya hapo unaweza enda
kwenye maabara sasa kufanya kipimo hicho kwa maelekezo kutoka kwa daktari.
Baadae daktari atakupa dawa sahihi ya kutumia ambayo inasisitizwa na wizara ya
afya kwa wakati huo. Kama ni ugonjwa mkubwa ambao bado upo katika hatua za
mwanzo, daktari ana uwezo wa kuutambua kuliko mtu ambae sio daktari, hii
itasaidia kuuwahi katika matibabu kabla haujafika mbali. Kujipa majukumu ya
daktari ama kuwapa majukumu hayo wataalamu wa maabara ni sawa na kujijengea
nyumba wakati ukijua wewe si fundi muashi, itakuangukia.
*culture ni
uoteshaji wa vimelea kwenye mazingira ambayo ni pendelevu kwa vimelea husika
kwa lengo la kutaka kuvifahamu. Kwa mfano wanataka kujua kama kwenye damu yako
kuna aina fulani ya vimelea basi wanachukua damu yako na kuiweka kwenye
mazingira ambayo vimelea vile vingeota kama kweli vipo kwenye damu yako.

Njema sana Dr.this is good staff
ReplyDeleteTuko pamoja daktari
DeleteEnter your comment...great!!
ReplyDeleteThanks
DeleteHii imekuwa desturi yetu kwa miaka mingi. Kwa namna moja au nyingine magonjwa mengi ambayo amefika hatua mbaya yangeweza kuzuilika kama tungekuwa na utaratibu wa kwenda hospitali.
ReplyDeleteMbali na hayo katika mazungumzo ya hapa na pale na baadhi ya watu nimepata sababu nyingine zinazowafanya watu kupenda kutumia maabara zetu za mitaani kama mbadala wa hospitali,ni kama moja msongamano wa watu hospitali ambayo hufanya watu kutumia siku nzima
Pili kuhisi wanachoumwa ni kidogo tu hakiihitaji sana kumuona daktari na tatu ni kutopata ushirikiano mzuri kutoka kwa watoa huduma za afya hospitalini. Kuboresha huduma za afya na kutoa elimu kwa jamii(kama Joseph Julius )itasaidia sana kupunguza tatizo hili
Ni kweli
DeleteGood article kaka
ReplyDeleteAsante sana kaka,
DeleteTupo pamoja
Safi kaka
ReplyDelete