Naamini katika maisha yetu wote tulishawahi kusikia ama
kufanya kitu ambacho tuliambiwa ni tiba pale tunapoumwa japo hakiingii akilini
kuwa tiba. Nakumbuka nilipokua nakua ulikua ukipata kipele jichoni tulichokiita
sekera uliambiwa ukaongelee kwenye tundu la choo na kitaisha, na kweli siku
chahe baada ya kuongelea kwenye tundu la choo kipele kile kiliisha; niliambiwa
pia jino liking’oka ili liote lingine basi sina budi kutupa jino lile
lililong’oka batini, na kweli nilipotupa jino lingne liliota, na wale watoto
wenye mapengo walikiri kutotupa meno yao batini; na mengine mengi.

Nimekua nikiongelea baadhi ya tiba ambazo ni za uongo lakini
najua kabisa kuna mtu akisoma anaona ninadanganya kwa sababu yeye amewahi
kutibiwa na moja ya tiba hizo na akajiona kupona. Wote tunaowaona wakitoa ushuhuda
kuhusu tiba ambazo ni za uwongo sio lazima wakawa wamepangwa na watoa huduma
zile, wengine ni waaminifu ambao kweli baada ya tiba zile walijisikia kupona.
Sio wote tunaowaona kwenye runinga wakifanyiwa maombi na kuanguka na kuanza
kupata degedege wanaigiza, wapo ambao wanafanya vile kweli bila kuigiza.
Naamini mnakumbuka wanasiasa walivyosimama mbele ya kamera na kusema
wanajisikia kupona dakika chache baada ya kunywa kikombe cha babu, naamini
walijisikia kupona kweli na walikua hawatudanganyi.
Yote hayo na mengine nitayataja yanaanguka kwenye neno la
kilatini “placebo” ambalo tafsiri
yake inafanana na msemo wa Kiswahili “kupaka
mafuta kwa mgongo wa chupa”. Kwenye fani hii ya tiba neno placebo lina maana ya tiba ambayo ni ya
uwongo ama isiyo na viwango lakini inampa mgonjwa unafuu. Hii ndiyo
inayowafanya wanaotoa tiba za uwongo kuendelea kung’ara na kutajirika kwani
wateja wao ni kweli kabisa wanajisikia vizuri wakipata huduma zao na
watawatafuta popote.
Mtu wa kwanza kufanya tafiti kuhusu swala hili alikuwa
mwingereza John Haygarth aliyekuwa daktari mstaafu, baada ya kuwepo kwa tiba
iliyohusisha kutumia vyuma kufyonza maumivu kutoka mwilini kama vile sumaku
inavyovuta vyuma, na wagonjwa walipona maumivu. Vyuma hivyo vilikuwa
vimetengenezwa na madini ya gharama na kuifanya tiba hiyo kuwa ya gharama.
Haygarth alichukua vyuma vilivyotumika kwa tiba hiyo na pia akatengeneza
vingine ambavyo havikutumia madini kama yale ya vile vya tiba. Cha kushangaza
wagonjwa walipona maumivu bila kujalisha wametumia vyuma gani. Haygarth alikuwa
sawa kufikiri kwamba kilichowaponya wagonjwa sio vile vyuma ila ni Imani ya
wagonjwa kwa vile vyuma.
Tafiti nyingine ilifanywa na Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo alieitwa Leonard Cobb miaka ya 1950 kwa watu waliokuwa wana maumivu ya
vifua kutokana na magonjwa ya moyo ambao kwa kipindi hicho walikuwa wanafanyiwa
upasuaji wa kifua na kufungwa mshipa mmojawapo wa damu ndani ya kifua ili
kuruhusu damu nyingi kwenda kwenye moyo na hivyo kuondoa maumivu. Cobb
aliwaweka wagonjwa wake waliokuwa wanasubiri upasuaji katika makundi mawili;wa
kundi la kwanza aliwapasua kifua na kuufunga mshipa huo kisha kukifunga kifua;
wa kundi la pili aliwapasua kifua ila hakufanya kitu chochote na kuwafunga
kifua ila aliwaaminisha kwamba amewafunga mshipa huo. Cha kushangaza ni kwamba
makundi ypote baada ya upasuaji yaliripoti kutopata maumivu ya kifua kama
ilivyo kuwa kabla ya upasuaji. Maumivu ya wagonjwa hawa hayakutibiwa na
upasuaji bali na Imani ya wagonjwa juu ya upasuaji ule, hii ndio placebo
Placebo haipo tu
kwenye tiba za uongo bali hata hospitalini ipo. Madaktari wawili wanaotoa tiba
zinazofanana sio lazima waponye wagonjwa kwa kiasi kinacholingana, ndio maana
upendo wa wagonjwa kwa madaktari tofauti haufanani. Lakini hospitalini
kinachotokea ni kwamba juu ya tiba ya ukweli inayopatikana, placebo inaongezeka tofauti na tiba
mbadala nyingi ambazo hazijathibitishwa ambazo huelemea kwenye placebo pekee. Tafiti zinaonesha kati ya
mambo yanayoongeza uponaji wa mgonjwa juu ya matibabu yanayopatikana
hospitalini ni kama vile kuvaa koti jeupe ukilinganisha na kuvaa t-shirt,
kuongea vizuri na wagonjwa, umaarufu wa daktari n.k.
Inafikiriwa kinachosababisha placebo kuwepo ni kwanza kuzoea
kuwa baada ya tiba huwa tunapata nafuu, kama vile mbwa waliozoeshwa kupigiwa
kengele kabla ya chakula wanapotoa udenda hata tu wakisikia kengele; pili ni
kiasi ambacho mgonjwa anaamini ataponywa na tiba fulani kinaendana na matokeo
ya tiba yake; ama zipo sababu zaidi ya hizi ambazo bado hazijajulikana bado
Sayansi imeweza kuliona hili na njia za kuthibitisha tiba za
kisayansi zimewekwa kiasi kwamba tofauti zinazoletwa na placebo zinafutwa kwanza na tiba inasimama kama tiba yenyewe. Kwa
mfano kwenye sayansi tukitaka kujua kama dawa X inatibu maumivu ya mgongo
tutawachukua watu wengi wenye maumivu ya mgongo na kisha tutaichukua dawa X
pamoja na dawa nyingine inayofanana kabisa na dawa X na tutawapa wagonjwa wale.
Wagonjwa wala wanaowapa dawa hizo hawatafahamu kama wanapewa dawa ya kweli ama
ile geresha inayofanana nayo na wote watakuwa kwenye mazingira yanayofanana.
Baadae tutaangalia ni kundi lipi lina wagonjwa wengi Zaidi waliopona maumivu ya
mgongo. Watakaopona kwa placebo
watakuwepo katika makundi yote hivyo watakaopona Zaidi ya hao watakuwa
wameponywa na dawa ile.
Unaweza kushangaa kwani hata kama ni placebo swala si kupona tu! Lakini kuna hatari zinazoweza
kuhusishwa na swala hili. Tafiti moja iliwachukua wagonjwa wa pumu na kisha
kuwapa tiba mbadala na wakasema wanajisikia pumu yao imekwisha na wanapumua
vizuri kabisa; lakini wakifanya vipimo, mapafu yao yanaonekana bado hayapo
vizuri na wanaweza kubanwa pumzi muda wowote na hivyo hawashauriwi kuachana na
dawa zao za kisasa. Kingine ni kwamba placebo
ipo vizuri Zaidi kwa dalili kama vile maumivu, homa, uchovu na kukosa hamu ya
chakula; hizi ni dalili ambazo zinaweza kuwepo kwa kuwa kuna ugonjwa mkubwa
zaidi, maumivu yanapotulizwa na placebo
huenda ikachelewesha kugundulika kwa ugonjwa uliopo.
Natumaini baada ya kujifunza haya hatutasimama kubishana
kwamba tiba fulani ni tiba sahihi kisa tu sisi wenyewe ni mashahidi aidha
tuliponywa nayo ama watu tunaowafahamu waliponywa. Njia sahihi ya kufahamu ni
kama tiba hiyo imefanyiwa tafiti kisayansi na kukubalika.
Maelezo yanatosheleza
ReplyDelete