Saturday, 15 October 2016

UONGO KUHUSU UTOAJI SUMU MWILINI



UONGO KUHUSU UTOAJI SUMU MWILINI
Neno SUMU limekuwa likitumika na matapeli kututisha kiafya na kutufanya tununue bidhaa zao za uongo. Nadhani hata wewe katika pita-pita zako umewahi kukutana na kikundi cha watu wakitangaza njia zao za kutoa sumu mwilini na kuuza huduma hiyo. Wataanza kwa kutuelezea jinsi gani maisha yetu yamezungukwa na sumu kuanzia vyakula, vinywaji, pombe, sigara, moshi wa magari, madawa ya hospitali, hewa tunayovuta kwamba vyote hivyo vina sumu. Watasema ndio maana siku hizi tunaumwa zaidi migongo, vichwa, mafua, n.k (hizi dalili kila mmoja ameshawahi kuzipata) na wataongeza mengine ya kututisha kama saratani. Baada ya hapo wataonesha bidhaa zao za kutoa sumu mwilini.
 Image result for utoaji sumu mwilini
Wanaweza kumwaga maji yenye rangi kwenye chombo na wakawaambia watu hiyo ni sumu na kisha wakachanganya na kemikali nyingine ambayo inasababisha yale maji ya rangi kupoteza rangi na kuwa maji masafi, “nunua hii dawa leo ujisafishe sumu mwilini mwako kama ulivyoona hapa” watawaambia watazamaji walioshangazwa na kile kitendo. Lakini ukweli ni kwamba hizi ni kemikali za kawaida tu ambazo zipo na kwa mtu aliyewahi kuhudhuria darasa la kemia akiwa sekondari anaweza kukumbuka walivyokuwa wanachanganya kemikali na rangi inapotea, na ninaamini zile dawa anazowauzia watu sio zile kemikali anazochanganya. Wengine huwaambia watu kuingiza miguu kwenye maji na baada ya muda maji yale yanabadilika rangi na hiyo rangi wanasema ni sumu inatoka kwenye mwili ya aliyeweka miguu. Ukichunguza vizuri utakuta wamechomeka vichuma ndani ya maji yale na wameunga kwenye chanzo cha nishati ya umeme mdogo; vyuma vikidumbukizwa kwenye kemikali na vikapitishwa umeme basi vinalika na kama vina kutu basi kutu itapukutika na maji yatachafuka, kwenye kemia hiki huitwa “electrolysis” na hakuna  sumu yoyote inayotoka mwilini.

Watu wa tiba mbadala wameiba hili neno “utoaji sumu mwilini” kutoka kwenye tiba ya kisasa, tiba ya kisayansi. Hospitalini utoaji sumu mwilini hufanywa kwa watu waliokunywa sumu, waliozidisha kiasi cha dawa ama pombe na katika hali hizi wagonjwa hawa huwa wanaumwa si utani.

Ni kweli tumezungukwa na kemikali nyingi, kemikali hizi huenda zikawa ni za asili ama za kutengezezwa. Lakini miili yetu imeumbika kujihami na kujisafisha na sumu ziingiazo mwilini kutoka nje pamoja na zile inazotengeneza yenyewe. Maini yetu ndiyo kiungo cha muhimu kabisa ukiongelea utoaji wa sumu mwilini, mafigo, mfumo wa chakula, mfumo wa upumuaji na mfumo wa limfu vyote vinafanya kazi kuhakikisha sumu zinatolewa nje ya mwili.

Mtu anaekwambia ule vyakula fulani ili kutoa sumu mwilini huo ni uongo, labda vyakula hivyo vikusaidie kwenye mambo mengine kiafya kwa mfano matunda na mboga-mboga kwa wingi hutupunguzia uwezekano wa kuugua magonjwa sugu. Ukikutana na mtu anakuuzia huduma ya kutoa sumu mwilini swali lako la kwanza liwe “nitajie majina ya hizo sumu” na la pili liwe “sumu hizo(hatozitaja maana hazipo) zinaletaje hayo magonjwa uliyoyataja?”. Matapeli hawa huishia kusema tu SUMU bila kuzitaja majina yake na hakuna uhusiano wa kile wananchoita sumu na magonjwa wanayoyasema yanatokana na hizo sumu.

Utapeli huu upo kwa kiasi kikubwa hapa kwetu kwani nilipojaribu kuingiza maneno “utoaji sumu mwilini” kwenye google, taarifa zote isipokuwa moja ya Wikipedia zilizokuja kwenye ukurasa wa kwanza ni taarifa za uwongo zenye dhamira ya kumuuzia msomaji hizi juice na vifaa vya kudanganyishia kutolea sumu mwilini, wataalamu wa afya hapa hatujafanya kazi yetu ipasavyo kuielimisha jamii. Mitandao mingi ilionekana kuuza juice inaitwa TREVO ambapo walisema nayo inatoa sumu. Kwenye mtandao wao wa trevocorporate.com wameandika juice hiyo imetengenezwa na vitu vya asili 174 na inakupa: nguvu za ziada, inakuongezea umakini wa akili, afya njema na kujisikia vizuri; wakaongeza kwamba TREVO inasaidia katika: kupunguza uzito, afya ya moyo, afya ya seli(hii sijui ni nini), afya ya mfumo wa chakula, mfumo wa fahamu, kinga ya mwili, afya ya macho, mifupa na viungo, kuzuia uzee(naomba nirudie: kuzuia uzee) na afya ya sukari kwenye damu. Tofauti ya hii na ile ya Loliondo ni hapa hakuna tu ndoto, maana nayo kama inatibu karibia kila kitu. Hata mimi ningependa maisha yawe rahisi hivi ila ukweli ni kwamba hayapo hivyo na natakiwa kusimama mbele ya ukweli.

Usitishwe na vitu ambavyo havipo, kula vizuri, fanya mazoezi, achana na tabia hatarishi kiafya, penda ku-check afya yako mara kwa mara na ufurahie maisha kwani duniani si tunapita wote.

0 comments:

Post a Comment