Saturday, 8 October 2016

SAYANSI: DAWA YA IMANI POTOFU



SAYANSI: DAWA YA IMANI POTOFU
Jumamosi iliyopita tulijionea kupitia vyombo vya habari na  mitandao mbalimbali ya kijamii picha za kutisha, kuumiza na kutesa mioyo yetu. Zilionekana picha za watu watatu, wanaume wawili na mwanake mmoja waliouwawa kikatili kwa kupigwa na baadae kuchomwa moto wamelala chini wameungua na hawatambuliki tena kwa sura. Watu wale walikuwa ni wafanyakazi wa kituo cha utafiti wa kilimo cha Selian, Selian Agricultural Research Institute (SARI) waliokuwa katika shughuli zao za utafiti wa udongo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo katika eneo lile. Watafiti Teddy Lumanga, Jaffari Mafuru na dereva wao Nicas Magazine wote waajiriwa wa kituo cha utafiti cha SARI iliarifiwa kwamba waliuawa kikatili kwa kupigwa na kukatwa-katwa  na silaha za jadi na kisha miili yao na gari lao kuchomwa moto katika kijiji cha Iringa-Mvumi wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwa kile wanakijiji walichodhani kuwa watu hawa walikuwa ni wanyonyaji wa damu za watu. Inasemekana mnamo majira ya saa sita na nusu za mchana jumamosi iliyopita, mwanamke mmoja aitwaye Cecilia Chimanga mwenye umri wa miaka 34 alitoa taarifa kwa wanakijiji wenzake kwamba amewaona watu ambao alizani kuwa ni wanyonyaji wa damu. Taarifa zile zilisambaa kwa haraka na kuongezewa na mchungaji wa kanisa la Christian Family Church aliyeishi kwenye kijiji kile aitwaye Patrick Mgonela mwenye umri wa miaka 46 ambae aliwatangazia wanakijiji kwamba kijiji chao kilikuwa kimevamiwa na wanyonya damu. Wanakijiji walikusanyika na ndipo wakatekeleza kitendo hicho cha kikatili.
 Image result for cartoon vampires
Inasikitisha kwenye karne ya 21 bado tunaamini kwamba kuna watu wananyonya damu. Hii ni moja ya Imani potofu kwa kiwango cha hali ya juu sana na hasara yake ndiyo kama ambayo yametokea huko Iringa-Mvumi. Watu wale waliouawa huenda wana watu wanaowategemea kwenye maisha kama wazazi waliozeeka ama wake/mme na watoto, na pia ni watu wa muhumu sana kwani kuishi bila tafiti ni sawa na kutembea gizani. Tafiti husaidia kwenye sekta mbalimbali: kwenye kilimo tafiti hutuambia udongo gani wafaa kulimwa mazao yapi ili tuzalishe Zaidi na tusipoteze nguvu, pesa na muda, hutuambia chanzo cha magonjwa mbalimbali ya mazao yetu mashambani na kutuletea dawa za kupambana nayo, n.k; kwenye sekta ya afya tafiti hutuambia nini kinasababisha ugonjwa fulani na kutupatia matibabu; hutuambia  njia mbalimbali za kujikinga na magonjwa; na katika sekta nyingine kadhalika.

Lakini hii si mara ya kwanza Imani potofu zimetuletea matatizo kwenye nchi yetu. Wazee wenye macho mekundu wameuawa kwa sababu ni wachawi, walemavu wa ngozi (Albino) wameuawa ili watu wapate mafanikio fulani, wengine wameuawa ili ngozi zao zichunwe. Haya ni yale ambayo yametokea kwa kiasi kikubwa ila pia kuna yale yanayompata mtu mmoja mmoja kama vile kuamini kwamba mtu fulani wa karibu yako aliyefariki hajafariki ila yupo ameshikiriwa sehemu fulani na mtu fulani unayemfahamu, kwamba kile mlichozika ni gogo ama mgomba ila mwenyewe yupo anafanyishwa kazi sehemu nyingine. Wengine wanaamini watu wana uwezo wa kupanda ungo (huwa sijui kwa nini sio beseni, sufuria ama diaba) na kwenda kokote watakako baada ya kufumba na kufumbua macho. Wengine wanaamini ugonjwa walionao umeletwa na mtu ama nguvu fulani ila sio asilia ya kawaida tu. Wengine wanaamini kuna watu wabaya huwa wanaangusha magari ili wanywe damu za abiria. Wengine wanaamini hawawezi kushinda mechi ya mpira kwa maandalizi bora bali kwa njia za kishirikina. Wengine wanaamini mtu anaweza kumuwekea dawa mpenzi wake ili afanye analoamriwa nae. Na ili kutoonekana napendelea upande mmoja wa jadi, wengine wanaamini watu wa dini wanaweza kukuondoa kwenye hayo niliyoyataja na hata kufufua waliokufa kama video za mchungaji mmoja maarufu nchini zinavyoonesha. Kwa kifupi naweza kuujaza huu ukurasa kwa kuandika vitu ambavyo tunaviamini na ambavyo hatuna navyo uthibitisho na vinatuletea shida zaidi.

Binafsi natofautiana na wengine kidogo kwa kwenda kwenye mzizi wa haya yote, naona chanzo cha haya yote ni kuwa nyuma kisayansi. Sayansi yapasa kuwa njia ya kufikiria Zaidi ya yale masomo ya darasani. Kwenye sayansi, asilia huchunguzwa kwa ukaribu na kuonesha tabia fulani ambazo hazibadilishwi na nguvu yoyote. Kwenye sayansi watu huja na mawazo ya aina yoyote yale kwa mfano tunaweza kujiuliza kama kuna watu wanakunywa damu za watu, kisha huenda mbele na kufanya majaribio kama hayo mawazo ni kweli. Majaribio hayo yanaweza kurudiwa popote pale duniani na yanatakiwa yalete majibu yanayofanana kama tu mazingira yalimofanyika yamefanana. Wanasayansi wakijiridhisha na majibu kwamba si kweli basi huachana na hayo mawazo mara moja bila kujarisha walikua na mapenzi kiasi gani na mawazo hayo. Sayansi inatufanya kufahamu damu inaundwa na nini na inatuambia kwamba damu zote za wanyama zinafanana kwa jinsi fulani.

Mafanikio ya sayansi yanaonekana na hayajifichi: tunaona ndege zinaruka, tunawasiliana kwenye simu, watu wameenda mwezini, tunaishi muda mrefu zaidi kuliko zamani, chanjo zimepunguza magonjwa na hata kuyafuta baadhi kwenye uso wa dunia,  n.k. Kwa upande wa pili, mengi yanayosemwa kwamba yanafanywa kwa nguvu za giza hayaonekani, kila anaye kuhadithia nae alisikia kwa mtu na kama aliona mwenyewe basi si muda mrefu mnamfunga kamba maana anakuwa anaanza kuonesha dalili za ugonjwa wa akili. Nilitegemea kwenye dunia ya leo ambamo sayansi imeonesha mafanikio ambayo kila mtu anayaona basi waganga wa kupiga ramli wangekosa kazi  na mawazo kama yale yaliyopelekea vifo huko Iringa-Mvumi ama mauaji ya albino yasingekuwepo. Haya ni matokeo ya kutojali mazingira ya ufundushaji wa sayansi mashuleni mfano kuvutana katika kujenga maabara na kuweka vifaa, kutowajali waalimu kuanzia ngazi ya chini kabisa, kujali vilabu vya pombe na mabanda ya kuangaliaizia ligi za mpira wa ulaya kuliko maktaba za kusomea na kukosa ajira kwa wale waliochukua masomo ya sayansi. Sayansi ndicho kitu cha muhimu kuliko vyote wanadamu tumewahi kuwa nacho tangu maisha yaanze. Tuwekeze kwenye sayansi kuepukana na Imani potofu zenye kutuletea matatizo.

3 comments:

  1. Mambo haya ni mzigo wa ujinga. Nilifanikiwa kusikiliza takwimu kuhusu elimu hususani ya Tanzania alizozitoa Mh.Zitto Kabwe katika mkutano mmoja ningependa kukushirikisha bofya link

    https://m.youtube.com/watch?v=4qXuPhG4S4I

    ReplyDelete
    Replies
    1. Copy na kupaste link hiyo kwenye browser yako

      Delete
  2. Ujinga ni ghali sana ,itachukua muda,pesa na watu kuutokomeza,ukielimika usi assume wote wameelimika ,wakati mwingine tunajisahau.(kabla hatujafanya tafiti au project kama hz tusi assume watu wote wameelimika ,tuwape tarifa na kuwaelimisha kwanza)

    RIP

    ReplyDelete