SAYANSI: DAWA YA
IMANI POTOFU
Jumamosi iliyopita tulijionea kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali
ya kijamii picha za kutisha, kuumiza na kutesa mioyo yetu.
Zilionekana picha za watu watatu, wanaume wawili na mwanake mmoja waliouwawa
kikatili kwa kupigwa na baadae kuchomwa moto wamelala chini
wameungua na hawatambuliki tena kwa sura. Watu wale walikuwa ni wafanyakazi wa
kituo cha utafiti wa kilimo cha Selian, Selian Agricultural Research Institute
(SARI) waliokuwa katika shughuli zao za utafiti wa udongo kwa ajili ya
maendeleo ya kilimo katika eneo lile. Watafiti Teddy Lumanga, Jaffari Mafuru na
dereva wao Nicas Magazine wote waajiriwa wa kituo cha utafiti cha SARI
iliarifiwa kwamba waliuawa kikatili kwa kupigwa na kukatwa-katwa na silaha za jadi na kisha miili yao na gari
lao kuchomwa moto katika kijiji cha Iringa-Mvumi wilayani Chamwino mkoani
Dodoma kwa kile wanakijiji walichodhani kuwa watu hawa walikuwa ni wanyonyaji
wa damu za watu. Inasemekana mnamo majira ya saa sita na nusu za mchana jumamosi
iliyopita, mwanamke mmoja aitwaye Cecilia Chimanga mwenye umri wa miaka 34
alitoa taarifa kwa wanakijiji wenzake kwamba amewaona watu ambao alizani kuwa
ni wanyonyaji wa damu. Taarifa zile zilisambaa kwa haraka na kuongezewa na
mchungaji wa kanisa la Christian Family Church aliyeishi kwenye kijiji kile
aitwaye Patrick Mgonela mwenye umri wa miaka 46 ambae aliwatangazia wanakijiji
kwamba kijiji chao kilikuwa kimevamiwa na wanyonya damu. Wanakijiji walikusanyika
na ndipo wakatekeleza kitendo hicho cha kikatili.
Inasikitisha kwenye karne ya 21 bado tunaamini kwamba kuna
watu wananyonya damu. Hii ni moja ya Imani potofu kwa kiwango cha hali ya juu
sana na hasara yake ndiyo kama ambayo yametokea huko Iringa-Mvumi. Watu wale
waliouawa huenda wana watu wanaowategemea kwenye maisha kama wazazi waliozeeka
ama wake/mme na watoto, na pia ni watu wa muhumu sana kwani kuishi bila tafiti
ni sawa na kutembea gizani. Tafiti husaidia kwenye sekta mbalimbali: kwenye
kilimo tafiti hutuambia udongo gani wafaa kulimwa mazao yapi ili tuzalishe
Zaidi na tusipoteze nguvu, pesa na muda, hutuambia chanzo cha magonjwa
mbalimbali ya mazao yetu mashambani na kutuletea dawa za kupambana nayo, n.k;
kwenye sekta ya afya tafiti hutuambia nini kinasababisha ugonjwa fulani na
kutupatia matibabu; hutuambia njia
mbalimbali za kujikinga na magonjwa; na katika sekta nyingine kadhalika.
Lakini hii si mara ya kwanza Imani potofu zimetuletea
matatizo kwenye nchi yetu. Wazee wenye macho mekundu wameuawa kwa sababu ni
wachawi, walemavu wa ngozi (Albino) wameuawa ili watu wapate mafanikio fulani,
wengine wameuawa ili ngozi zao zichunwe. Haya ni yale ambayo yametokea kwa
kiasi kikubwa ila pia kuna yale yanayompata mtu mmoja mmoja kama vile kuamini
kwamba mtu fulani wa karibu yako aliyefariki hajafariki ila yupo ameshikiriwa
sehemu fulani na mtu fulani unayemfahamu, kwamba kile mlichozika ni gogo ama
mgomba ila mwenyewe yupo anafanyishwa kazi sehemu nyingine. Wengine wanaamini
watu wana uwezo wa kupanda ungo (huwa sijui kwa nini sio beseni, sufuria ama
diaba) na kwenda kokote watakako baada ya kufumba na kufumbua macho. Wengine
wanaamini ugonjwa walionao umeletwa na mtu ama nguvu fulani ila sio asilia ya
kawaida tu. Wengine wanaamini kuna watu wabaya huwa wanaangusha magari ili
wanywe damu za abiria. Wengine wanaamini hawawezi kushinda mechi ya mpira kwa
maandalizi bora bali kwa njia za kishirikina. Wengine wanaamini mtu anaweza
kumuwekea dawa mpenzi wake ili afanye analoamriwa nae. Na ili kutoonekana
napendelea upande mmoja wa jadi, wengine wanaamini watu wa dini wanaweza
kukuondoa kwenye hayo niliyoyataja na hata kufufua waliokufa kama video za
mchungaji mmoja maarufu nchini zinavyoonesha. Kwa kifupi naweza kuujaza huu
ukurasa kwa kuandika vitu ambavyo tunaviamini na ambavyo hatuna navyo
uthibitisho na vinatuletea shida zaidi.
Binafsi natofautiana na wengine kidogo kwa kwenda kwenye
mzizi wa haya yote, naona chanzo cha haya yote ni kuwa nyuma kisayansi. Sayansi
yapasa kuwa njia ya kufikiria Zaidi ya yale masomo ya darasani. Kwenye sayansi,
asilia huchunguzwa kwa ukaribu na kuonesha tabia fulani ambazo hazibadilishwi
na nguvu yoyote. Kwenye sayansi watu huja na mawazo ya aina yoyote yale kwa
mfano tunaweza kujiuliza kama kuna watu wanakunywa damu za watu, kisha huenda
mbele na kufanya majaribio kama hayo mawazo ni kweli. Majaribio hayo yanaweza
kurudiwa popote pale duniani na yanatakiwa yalete majibu yanayofanana kama tu
mazingira yalimofanyika yamefanana. Wanasayansi wakijiridhisha na majibu kwamba
si kweli basi huachana na hayo mawazo mara moja bila kujarisha walikua na
mapenzi kiasi gani na mawazo hayo. Sayansi inatufanya kufahamu damu inaundwa na
nini na inatuambia kwamba damu zote za wanyama zinafanana kwa jinsi fulani.
Mafanikio ya sayansi yanaonekana na hayajifichi: tunaona
ndege zinaruka,
tunawasiliana kwenye simu, watu wameenda mwezini, tunaishi muda mrefu zaidi kuliko
zamani, chanjo zimepunguza magonjwa na
hata kuyafuta baadhi kwenye
uso wa dunia, n.k. Kwa upande wa pili, mengi yanayosemwa
kwamba yanafanywa kwa nguvu za giza hayaonekani, kila anaye kuhadithia nae alisikia kwa mtu na kama aliona mwenyewe basi si muda
mrefu mnamfunga kamba maana anakuwa anaanza kuonesha dalili za ugonjwa wa akili.
Nilitegemea kwenye dunia ya leo ambamo sayansi imeonesha mafanikio ambayo kila
mtu anayaona basi waganga wa kupiga ramli wangekosa kazi na mawazo kama yale yaliyopelekea vifo huko
Iringa-Mvumi ama mauaji ya albino yasingekuwepo. Haya ni matokeo ya
kutojali mazingira ya ufundushaji wa sayansi mashuleni mfano kuvutana katika
kujenga maabara na kuweka vifaa, kutowajali waalimu kuanzia ngazi ya chini
kabisa, kujali vilabu vya pombe na mabanda ya kuangaliaizia ligi za mpira wa
ulaya kuliko maktaba za kusomea na kukosa ajira kwa wale waliochukua masomo ya
sayansi. Sayansi ndicho kitu cha muhimu kuliko vyote wanadamu tumewahi kuwa
nacho tangu maisha yaanze. Tuwekeze kwenye sayansi kuepukana na Imani potofu
zenye kutuletea matatizo.
Mambo haya ni mzigo wa ujinga. Nilifanikiwa kusikiliza takwimu kuhusu elimu hususani ya Tanzania alizozitoa Mh.Zitto Kabwe katika mkutano mmoja ningependa kukushirikisha bofya link
ReplyDeletehttps://m.youtube.com/watch?v=4qXuPhG4S4I
Copy na kupaste link hiyo kwenye browser yako
DeleteUjinga ni ghali sana ,itachukua muda,pesa na watu kuutokomeza,ukielimika usi assume wote wameelimika ,wakati mwingine tunajisahau.(kabla hatujafanya tafiti au project kama hz tusi assume watu wote wameelimika ,tuwape tarifa na kuwaelimisha kwanza)
ReplyDeleteRIP