Sunday, 18 December 2016



Marehemu Langa aliwahi kuimba kwamba “ukitaka kumficha mwafrika weka ujumbe kwenye vitabu”. Langa alimaanisha kuwa sisi hatuna tamaduni ya kupenda kupekua-pekua vitabu. Hili siyo jambo jema lakini kizuri Zaidi ni kwamba hii tabia si ya kurisi kama tulivyorisi rangi zetu bali tunaweza kubadilika na kuutengeneza utamaduni huu miongoni mwetu baada tu ya kutambua umuhimu wake na kutengeneza mifumo ya kuwezesha hilo kutokea.
 Image result for reading culture
Binafsi naamini kupitia kusoma ni njia kuu ya kujitoa kwenye matatizo tuliyonayo. Ukweli wa hili unajidhihirisha hata kwenye historia. Kipindi mtu mweusi alipoishi kama mtumwa nchini Marekani ni kipindi ambacho pia hakuruhusiwa kujua kusoma wala kuandika, sheria zao zilikataza kabisa mtu mweusi kupelekwa shule na bwana wake. Walijua kabisa mtu yule alikuwa ana akili na kama angejua kusoma basi hiyo ingekuwa kama tochi yake kuona yale asiyotakiwa kuyaona na huo ungekuwa mwisho wa unyonyaji na ukandamizaji ulioendelea. Hata vuguvugu la kutafuta haki za watu weusi lililetwa na wale wachache ambao kwa bahati ya mtende waliweza kujua kusoma. Huko Afrika ya Kusini pia makaburu walibana elimu kwa watu weusi ukilinganisha na wao wenyewe, hata Mandela mwenyewe alipata elimu kwa sababu baba yake alikuwa mshauri wa chifu na alipofariki alilelewa na chifu. Hata hapa kwetu wakoloni hawakutoa elimu kwa faida yetu bali kwa faida zao pale ilipowabidi kama vile kusomesha watoto wa machifu ili waelewane na machifu.

Mfano mkubwa kabisa katika kuonesha kusoma kunaweza kubadilisha maisha ya mtu ni wa kijana mmalawi aitwaye William Kamkwamba. Kamkwamba alizaliwa kwenye familia masikini huko kijijini kwao Masitala karibu na jiji la Kasungu. Alipokuwa anaingia kuanza elimu yake ya sekondari, Malawi ilikuwa imekumbwa na mafuriko yaliyoambatana na njaa kitu ambacho kilimfanya baba yake ashindwe kumlipia ada ya shule. Kamkwamba alibaki nyumbani ila hakukaa tu bali alipenda kwenda maktaba kujisomea ili angalau awe sambamba na wenzake pindi ada itakapopatikana na akarudi shule. Alisoma vitabu mbalimbali ila kilichobadilisha maisha yake anasema kiliitwa Explaining Physics ambacho kilieleza jinsi kata upepo inavyofanya kazi na kutengeneza umeme. Kwa kutumia kitabu hicho aliweza kutengeneza kata upepo kwa kuunga-unga kutoka kwenye vitu alivyookota jalalani likatoa umeme akawasha taa kwao na akatumia kuchaji simu za wanakijiji. Aliwahi pia kutengeneza bayogesi na pampu ya kuvuta maji kutoka kisimani japo havikufanikiwa kutokana na kukosa vifaa. Cha ajabu shule za serikali za Malawi zilipoombwa kumuingiza aendelee na elimu yake zilisema alikuwa ana umri mkubwa, na hata serikali ya Malawi haikujua wala haikumsaidia chochote katika kukuza kipaji chake; na hata alipokutana na raisi Bingu Wa Mutharika alipokuwa amealikwa kwenye mkutano mmoja huko Afrika Kusini ndio ilikuwa mara ya kwanza rais anamuona William na kwa mara ya kwanza anasikia habari zake. William alipata scholarship kwenye shule ya international na baadae akaenda kusoma African Leadership Academy kabla ya kwenda kusoma uinjinia chuo kikuu cha Dartmouth nchini Marekani.

Wengi mara ya mwisho kusoma huwa ni pale tukiwa shuleni na mara nyingi tunasoma field zinazotuhusu tu. Ni vigumu kumkuta mwanafunzi wa udaktari labda anasoma kitabu cha historia, filosofia ama astrofizikia. Lakini hatuwezi kuzungumza kuwa hatuna utamaduni wa kupenda kusoma bila kugusa upande wa pili kwamba hatuna pia utamaduni wa kuuandikia umma (tunao wataalamu wanaoandika sana machapisho ya tafiti ila ni katika kada zao za elimu, tofauti na kuuandikia umma). Nikitembelea maduka ya vitabu, vitabu vingi ninavyoviona huwa ni vya kujifunzia mashuleni  na vingine huwa vimetoka nje ya nchi ambavyo huwa vinawaelekeza watu jinsi ya kupata mafanikio maishani. Vilivyoandikwa na watanzania wenzetu huwa ni kimoja kimoja ukiachilia mbali vijitabu vyenye stori za watu wanaodai wamewahi kupelekwa kuzimu na mambo mengine ya uchawi ambayo huwa ni uwongo tu. Huwa najiuliza kama tunataka kujifunza kuhusu kufanikiwa katika mazingira ya kitanzania kwanini watu kama akina Mo Dewji, Mengi ama Bakhresa wasituandikie tuyasome mawazo yao. Kwanini wazee waliopata bahati ya kusoma enzi za mwalimu wasituandikie mawazo yao kuhusu hali ya nchi inavyokwenda. Kwanini wanasayansi wachache tulio nao wasituandikie kuhusu maendeleo ya sayansi ama nini kifanyike kuhusu sayansi nchini kwetu. Watu waliofanikiwa kwenye sekta zao kama akina Platinums na Samata waweza kuongea na wengine wanaotaka kuwa kama wao kupitia vitabu na sio kwa kuwafollow tu kwenye instagram.

Ni dhahir pia hatujaweka mazingira mazuri yenye kuamsha utamaduni wa kupenda kusoma. Tukijenga nyumba zetu nzuri za gharama tunaweka sebure nzuri ili wageni watupe sifa ila tunasahau kuweka maktaba na kuzijaza vitabu. Kama kuna kitu sijawahi kusikia serikali hata ikikiongelea huwa ni maktaba zake, mara ya mwisho naingia maktaba ya mkoa wa mwanza ilikuwa mwaka 2011  ila vitabu vyake vilikuwa ni vya muda mrefu vilivyochoka na kulikuwa na kiingilio. Wengi waliokuwa mule walikuwa ni wanafunzi wa sekondari waliokwenda pale ili kupata utulivu wa kujisomea mambo yao ya shuleni. Vitabu vingi huwa tunapewa kama misaada japo tuna watu wenye uwezo wa kulipia watu mamilioni ya pesa waangalie mpira bure zaidi ya mara moja. Kila mtaa wetu una banda la kuangalizia mpira unaorushwa kutoka upande mwingine wa dunia na tunalipia ila hatuwezi kuweka hata ka maktaba cha watoto wadogo. Mashuleni kwetu si tu kwamba watoto wanakosa vitabu vya kujifunzia bali wakati mwingine hata mwalimu anakosa kitabu cha kufundishia

Mwaka 2013 nilipoona kuna ugumu wa kupata vitabu hapa nchini nilisaidiwa na rafiki yangu kuagiza kifaa kwa jili ya kusomea kiitwacho kindle. Kilikuja bila kava na nikaamua kulitafuta kava lake kwenye maduka ya jiji letu kuu la Dar es salaam. Nilishangazwa pale nilipoona kuwa maduka yoote niliyotembelea yakiwemo ya kariakoo, mlimani city, posta na kwingine hayakuifahamu kindle na hawajawahi hata kuisikia. Mmoja kati ya wauzaji aliniuliza “unasema unatafuta kinu?”. Ila jibu la kwanini kifaa hiki hakikujulikana kwenye maduka haya miaka takribani 6 baada ya kuanza kutolewa na kampini la Amazon ni kwa sababu hakina kazi nyingine zaidi ya kusomea tu. Simu za gharama zikitoka huwa zinapatikana nchini ndani ya mwezi huohuo ziliotolewa. Tunaishi kwenye dunia ya kiteknolojia zaidi ya wakati wowote duniani, na kitu muhimu ni nini kimo ndani ya vichwa vyetu. Tutaweza kuendana na dunia hii kwa kupenda kuongeza ujuzi na njia ya kufanya hilo ni kwa kusoma. Tukuze utamaduni wa kupenda kusoma.

TUJENGE UTAMADUNI WA KUPENDA KUSOMA

Saturday, 26 November 2016



Binafsi nikisikia neno maombi kumbukumbu inayokuja kichwani huwa si ya kupendeza kabisa. Mnamo mwaka 2002 nilishuhudia mtoto mdogo anagongwa na gali. Inaonekana alikuwa na mama yake na walikuwa wamekuja eneo lile kwa ajili ya huduma za kiroho maana ilikuwa ni barabara ya kuvuka kutokea kanisani. Baada ya kumgonga gali lile lilikimbia na watu waliokuwa eneo lile wengi walikuwa wamekuja kanisani pia. Walimuokota yule mtoto aliyekuwa amepoteza fahamu na kisha kumpeleka kanisani kwa ajili ya kuombewa ili aponywe. Nilichosikia kesho yake ni kwamba yule mtoto alifariki. Baada ya kujifunza mambo ya afya na uponyaji (kwa tiba za kisasa lakini) miaka mingi baadae, sijaacha kuhisi nini kilimfanya mtoto yule kufariki na kama matokeo yangebadilika iwapo angewahishwa hospitalini. Mfano, baada ya kupoteza fahamu mtoto yule labda alizibwa hewa na ulimi wake; mchungaji sidhani kama angeweza kumfungua mdomo ili auweke vizuri ulimi wake. Ama labda hata kama angepelekwa hospitali hakuna ambalo lingebadilika, sina uhakika ila ninachoamini ni kwamba wangefanya kitu cha msingi Zaidi ya mchungaji. Huu ni mfano hasi ila pia ninao mfano chanya: mmoja kati ya mama zangu wadogo aliwahi kuwa anasumbuliwa sana na madonda ya tumbo kwa muda mrefu. Anasema alitumia dawa ila hakupata nafuu. Siku moja akiwa amelala aliamka usiku wa manane kutokana na maumivu ya tumbo na kwenye redio alimsikia mchungaji anahubiri na akasema kama kuna sehemu inauma uishike na itapona; basi alishika tumbo  na tangu siku hiyo yeye amepona madonda ya tumbo.
Image result for mchungaji dawa ya mbu
Huenda wengi hatufahamu ila maombi yakitumika kama tiba basi hiyo nayo ni tiba mbadala kwani maana ya tiba mbadala ni tiba zote ambazo hazipo kwenye tiba za kisasa, tiba za kisayansi, tiba za magharibi. Tiba ya maombi hutumia “nguvu” inayotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ambae ndiye mgonjwa na kumponya. Neno nguvu kama linavyotumika hapa sio katika ile maana ya nguvu kama ile nguvu ya umeme kusukuma mashine ila ni nguvu ikiwa  na maana ya kiroho, nguvu ambayo sisi hatuwezi kuiona ila wanasema ipo.

Ni kweli maombi yana uwezo wa kuponya kupitia iyo nguvu? Ama kuna namna ya kuyaelezea mambo? Tafiti zilizofanywa kuliangalia hili zimeonesha kwamba hakuna nguvu iliyopo bali kilichopo ni kwamba maombi yana placebo kubwa sana (huko nyuma nimewahi kuelezea maana ya placebo). Wagonjwa wakiwa wanaombewa na wanafahamu kuwa wanaombewa basi wanapata faraja na kuhisi upendo, hiyo huweza kuharakisha uponaji wao ila pia huweza kuwafanya wajisikie vizuri na kuhisi kupona hata kama bado wana ugonjwa. Wagonjwa wanaoombewa ila hawajui kama wanaombewa hawapati mabadiliko yoyote yale yanayotokana na maombi yale. Huko USA mwaka 2006 yalichapishwa matokeo ya tafiti iliyofanywa kwa miaka 10 na kugharimu dola za kimarekani milioni 2.5. Utafiti huo ulihusisha wagonjwa 10,000 waliokuwa wamefanyiwa opasuaji wa mishipa ya moyo kwenye hospitali sita za nchi hiyo ikiwemo Havard. Wagonjwa hao waligawiwa kwenye makundi mawili na kundi moja likaombewa kwa miaka yote iyo kumi ila kundi jingine halikuombewa. Hakuna mgonjwa aliyejua kundi alimo. Mwisho wa siku ilionekana makundi yote mawili yalikuwa na maendeleo sawa tu na hakukuwa na tofauti iliyoletwa na maombi. Imani ya watu juu ya maombi ndiyo ishu hapa na sio nguvu ya waponyaji.

Kila tukifungua runinga zetu tunawaona watu wengi ambao wanatoa ushuhuda juu ya kuponywa kwao na wachungaji wanaomiliki kanisa na kipindi kinachooneshwa. Wengine hata wanasema walikuwa na magonjwa makubwa kama saratani ama maambukizi ya VVU na wameponywa. Hawa huwa tunawaona mara moja tu na hatuwafatilii wanakwenda wapi baadae, kama kweli walikuwa na magonjwa makubwa kama haya na wakaamini wameponywa na maombi na wakaachana na tiba nyingine basi tukiwatafuta miaka ya baadae tutakutana na vyeti vyao vya kifo tu. Mtu akisema ana saratani swali la kwanza lapaswa kuwa amejuaje na kama hajafanya vipimo mfano kutoa kinyama kilichopelekwa kuchunguzwa basi huyo ni muongo tu. Wachungaji wengine wameenda mbali na wanadai wanaweza kufufua hata watu waliokufa. Japo sijawahi kusikia hao waliokufa nani aliwathibitisha kwamba wamekufa, na sijaona mtu akiwahoji walipokufa walienda wapi. Ila hata kama wakithibitishwa, anaewathibitisha ni mwanadamu pia. Yule mtoto wa panya road aliezinduka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Temeke akizaniwa amefariki ni mfano tosha, kama ingetokea mchungaji amemuombea kabla basi angechukua sifa za kufufua zisizomstahili. Ila wenye uwezo wa kufufua watu, tuwashauri watembelee vyumba vya maiti mahospitalini kwani huko ndiko waliko wengi waliofariki.

Mtu hakatazwi kuombewa ila maombi hayapaswi kuchukua nafasi ya tiba kwani kuna matatizo mengi yatatokea. Waombeaji pia baada ya kuombea hawatoi hata njia za kujizuia na magonjwa mfano kulala kwenye neti, kunawa mikono, ngono salama, kufanya mazoezi na kadhalika, wao wanasubiri tu uumwe ndio watoe huduma. Pia tukumbuke maombi yamekuwepo tangu kitambo sana, tangu enzi za Yesu ila tiba za kweli zimetokea ndani ya miaka 100 tu iliyopita kutokana na kukua kwa sayansi. Mfano zamani ukiwa na kifua kikuu basi una wigo mfinyu sana wa kuishi na maombi yalikuwepo, ila kwa sasa kuna dawa na utapona.

MAOMBI KAMA TIBA

Saturday, 12 November 2016



Naamini katika maisha yetu wote tulishawahi kusikia ama kufanya kitu ambacho tuliambiwa ni tiba pale tunapoumwa japo hakiingii akilini kuwa tiba. Nakumbuka nilipokua nakua ulikua ukipata kipele jichoni tulichokiita sekera uliambiwa ukaongelee kwenye tundu la choo na kitaisha, na kweli siku chahe baada ya kuongelea kwenye tundu la choo kipele kile kiliisha; niliambiwa pia jino liking’oka ili liote lingine basi sina budi kutupa jino lile lililong’oka batini, na kweli nilipotupa jino lingne liliota, na wale watoto wenye mapengo walikiri kutotupa meno yao batini; na mengine mengi.
 Image result for placebo
Nimekua nikiongelea baadhi ya tiba ambazo ni za uongo lakini najua kabisa kuna mtu akisoma anaona ninadanganya kwa sababu yeye amewahi kutibiwa na moja ya tiba hizo na akajiona kupona. Wote tunaowaona wakitoa ushuhuda kuhusu tiba ambazo ni za uwongo sio lazima wakawa wamepangwa na watoa huduma zile, wengine ni waaminifu ambao kweli baada ya tiba zile walijisikia kupona. Sio wote tunaowaona kwenye runinga wakifanyiwa maombi na kuanguka na kuanza kupata degedege wanaigiza, wapo ambao wanafanya vile kweli bila kuigiza. Naamini mnakumbuka wanasiasa walivyosimama mbele ya kamera na kusema wanajisikia kupona dakika chache baada ya kunywa kikombe cha babu, naamini walijisikia kupona kweli na walikua hawatudanganyi.

Yote hayo na mengine nitayataja yanaanguka kwenye neno la kilatini “placebo” ambalo tafsiri yake inafanana na msemo wa Kiswahili “kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa”. Kwenye fani hii ya tiba neno placebo lina maana ya tiba ambayo ni ya uwongo ama isiyo na viwango lakini inampa mgonjwa unafuu. Hii ndiyo inayowafanya wanaotoa tiba za uwongo kuendelea kung’ara na kutajirika kwani wateja wao ni kweli kabisa wanajisikia vizuri wakipata huduma zao na watawatafuta popote.

Mtu wa kwanza kufanya tafiti kuhusu swala hili alikuwa mwingereza John Haygarth aliyekuwa daktari mstaafu, baada ya kuwepo kwa tiba iliyohusisha kutumia vyuma kufyonza maumivu kutoka mwilini kama vile sumaku inavyovuta vyuma, na wagonjwa walipona maumivu. Vyuma hivyo vilikuwa vimetengenezwa na madini ya gharama na kuifanya tiba hiyo kuwa ya gharama. Haygarth alichukua vyuma vilivyotumika kwa tiba hiyo na pia akatengeneza vingine ambavyo havikutumia madini kama yale ya vile vya tiba. Cha kushangaza wagonjwa walipona maumivu bila kujalisha wametumia vyuma gani. Haygarth alikuwa sawa kufikiri kwamba kilichowaponya wagonjwa sio vile vyuma ila ni Imani ya wagonjwa kwa vile vyuma.

Tafiti nyingine ilifanywa na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alieitwa Leonard Cobb miaka ya 1950 kwa watu waliokuwa wana maumivu ya vifua kutokana na magonjwa ya moyo ambao kwa kipindi hicho walikuwa wanafanyiwa upasuaji wa kifua na kufungwa mshipa mmojawapo wa damu ndani ya kifua ili kuruhusu damu nyingi kwenda kwenye moyo na hivyo kuondoa maumivu. Cobb aliwaweka wagonjwa wake waliokuwa wanasubiri upasuaji katika makundi mawili;wa kundi la kwanza aliwapasua kifua na kuufunga mshipa huo kisha kukifunga kifua; wa kundi la pili aliwapasua kifua ila hakufanya kitu chochote na kuwafunga kifua ila aliwaaminisha kwamba amewafunga mshipa huo. Cha kushangaza ni kwamba makundi ypote baada ya upasuaji yaliripoti kutopata maumivu ya kifua kama ilivyo kuwa kabla ya upasuaji. Maumivu ya wagonjwa hawa hayakutibiwa na upasuaji bali na Imani ya wagonjwa juu ya upasuaji ule, hii ndio placebo

Placebo haipo tu kwenye tiba za uongo bali hata hospitalini ipo. Madaktari wawili wanaotoa tiba zinazofanana sio lazima waponye wagonjwa kwa kiasi kinacholingana, ndio maana upendo wa wagonjwa kwa madaktari tofauti haufanani. Lakini hospitalini kinachotokea ni kwamba juu ya tiba ya ukweli inayopatikana, placebo inaongezeka tofauti na tiba mbadala nyingi ambazo hazijathibitishwa ambazo huelemea kwenye placebo pekee. Tafiti zinaonesha kati ya mambo yanayoongeza uponaji wa mgonjwa juu ya matibabu yanayopatikana hospitalini ni kama vile kuvaa koti jeupe ukilinganisha na kuvaa t-shirt, kuongea vizuri na wagonjwa, umaarufu wa daktari n.k.

Inafikiriwa kinachosababisha placebo kuwepo ni kwanza kuzoea kuwa baada ya tiba huwa tunapata nafuu, kama vile mbwa waliozoeshwa kupigiwa kengele kabla ya chakula wanapotoa udenda hata tu wakisikia kengele; pili ni kiasi ambacho mgonjwa anaamini ataponywa na tiba fulani kinaendana na matokeo ya tiba yake; ama zipo sababu zaidi ya hizi ambazo bado hazijajulikana bado

Sayansi imeweza kuliona hili na njia za kuthibitisha tiba za kisayansi zimewekwa kiasi kwamba tofauti zinazoletwa na placebo zinafutwa kwanza na tiba inasimama kama tiba yenyewe. Kwa mfano kwenye sayansi tukitaka kujua kama dawa X inatibu maumivu ya mgongo tutawachukua watu wengi wenye maumivu ya mgongo na kisha tutaichukua dawa X pamoja na dawa nyingine inayofanana kabisa na dawa X na tutawapa wagonjwa wale. Wagonjwa wala wanaowapa dawa hizo hawatafahamu kama wanapewa dawa ya kweli ama ile geresha inayofanana nayo na wote watakuwa kwenye mazingira yanayofanana. Baadae tutaangalia ni kundi lipi lina wagonjwa wengi Zaidi waliopona maumivu ya mgongo. Watakaopona kwa placebo watakuwepo katika makundi yote hivyo watakaopona Zaidi ya hao watakuwa wameponywa na dawa ile.

Unaweza kushangaa kwani hata kama ni placebo swala si kupona tu! Lakini kuna hatari zinazoweza kuhusishwa na swala hili. Tafiti moja iliwachukua wagonjwa wa pumu na kisha kuwapa tiba mbadala na wakasema wanajisikia pumu yao imekwisha na wanapumua vizuri kabisa; lakini wakifanya vipimo, mapafu yao yanaonekana bado hayapo vizuri na wanaweza kubanwa pumzi muda wowote na hivyo hawashauriwi kuachana na dawa zao za kisasa. Kingine ni kwamba placebo ipo vizuri Zaidi kwa dalili kama vile maumivu, homa, uchovu na kukosa hamu ya chakula; hizi ni dalili ambazo zinaweza kuwepo kwa kuwa kuna ugonjwa mkubwa zaidi, maumivu yanapotulizwa na placebo huenda ikachelewesha kugundulika kwa ugonjwa uliopo.

Natumaini baada ya kujifunza haya hatutasimama kubishana kwamba tiba fulani ni tiba sahihi kisa tu sisi wenyewe ni mashahidi aidha tuliponywa nayo ama watu tunaowafahamu waliponywa. Njia sahihi ya kufahamu ni kama tiba hiyo imefanyiwa tafiti kisayansi na kukubalika.

PLACEBO