BODABODA: CHANZO
KIKUBWA CHA AJALI KILICHOSAHAULIKA
Kuna kipindi niliishi sehemu ambayo daladala za kufika kule
ziliisha mida ya saa mbili za usiku na usafiri uliobaki ulikua ni pikipiki
maarufu kama “bodaboda” ama labda utembee. Shughuli niliyokuwa nafanya
iliniradhimu kurudi usiku mara kwa mara na sikuwa na budi kutumia bodaboda kwa
usafiri. Siku moja nilipanda bodaboda ya kijana mmoja ambae kiumri anaweza kuwa
kati ya miaka 17 hadi 20, naikumbuka sura yake, alikua amenyoa kiduku na hakuwa
na kofia (Helmet) ya kwake mwenyewe
wala ya abiria wake. Barabarani alikimbia kwa mwendo wa kasi sana kiasi cha
mimi kumwambia apuguze mwendo. Alipofika sehemu ambayo alitakiwa ahamie upande
mwingine wa barabara ili aende mahali nilipomuelekeza, alifanya hivyo pasi hata
na kuwasha taa za kuashiria; kulikuwa na pikipiki nyingine katika upande wa
pili wa barabara ambayo nayo ilikuwa katika mwendo mkali pia, ilibaki kidogo
sana pikipiki zile kugongana. Yule kijana alienibeba mimi akasimama na mwenzie
akasimama wakaanza kutukanana na mimi nikiwa pembeni najiuliza kama naamini
katika bahati ama la! uku nikiuhisi moyo unavyokita na mikono inatetemeka,
nikajua ilibakia kidogo sana nijishuhudie kwenye ajali ya bodaboda nikiwa kama
abiria. Yule bwana mwingine alilalamika sisi hatukuwa tumewasha taa ya
kuashiria tunavuka lakini cha ajabu yule dereva wangu alikua analalamika
akisema “watu wengine bwana, hivi we huwezi kuona kama mimi navuka upunguze
mwendo?mpaka niwashe taa?”.

Ajali za barabarani zimeongezeka sana siku hizi
ukilinganisha na zamani hasa kwenye nchi za pato la chini kama yetu hii na zile
za pato la kati. Kukua kwa miji na viwanda katika nchi hizi ndiko kunakopelekea
kuongezeka kwa ajali hizi; namba ya vyombo vya moto imekua kwa kasi kubwa
kuzidi kasi ya kuendeleza barabara bora na za kutosha. Pamoja na hali mbaya ya
barabara zetu, kutotumia kinga kama vile kofia na mikanda, huduma mbovu kwa
majeruhi na kutotii sharia za barabarani vinachangia matatizo yanayoambatana na
ajali kwenye nchi hizi. Kiasi cha ajali kwenye nchi zinazoendelea ni zaidi ya maradufu
ukilinganisha na zile zilizoendelea na tafiti zinaonesha kwamba uwezekano wa
kufa kwenye ajali ukiwa hapa nchini kwetu ni mara 20 hadi 30 zaidi ya ukiwa
nchini marekani ama nchi za ulaya.
Kuongezeka kwa wingi wa pikipiki hapa nchini kumekuwa na
faida kwa upande mmoja ambapo vijana wamejipatia ajira ya bodaboda na usafiri
huo umejidhihirisha kuwa wa haraka na nafuu ukiringanishwa na usafiri mwingine
wa kukodi kama vile taxi. Kwa hapa nchini bodaboda zimeajiri vijana wengi kiasi
cha kuwafanya wanasiasa kuliona kundi hili ni muhimu kwa wingi wa kura pale
uchaguzi unapokuja (kama ilivyo kwa makundi mengine muhimu kwao, hupotea
vinywani mwao pale uchaguzi ukishapita). Kwa upande mwingine pikipiki ndizo
zinaongoza kwa ajari za barabarani hapa nchini, kwa kusababisha zaidi ya nusu
ya ajali za barabarani. Tafiti moja iliyofanywa kwenye hospitali za MOI, Amana,
Mwananyamala , Temeke, Tumbi na hospitali ya mkoa wa Morogoro ilionesha zaidi
ya nusu ya ajali za barabarani zinazowapata watu waliofikishwa kwenye hospitali
hizo zimesababishwa na pikipiki. Taffiti nyingine iliyofanywa uko katika
hospitali ya rufaa ya Bugando mkoani Mwanza ilionesha hivyo pia. Ajali hizi
zimeplekea vifo na ulemavu wa kudumu kwa nguvu kazi ya taifa ikizingatiwa
kwamba wengi wanaopata ajali hizi ni wa umri kati ya miaka 18 na 45.
Tumekua tukishuhudia jitihada mbali mbali wakati ajali za
mabasi zinapozidi nchini, jitihada hizo ni nzuri na huwa zinapelekea kupungua
kwa ajali za mabasi kwa kiasi fulani. Ni vyema pia jitihada kama hizo zikawekwa
kwenye upande wa pikipiki. Madereva wengi wa bodaboda wanaoumia wakati wa ajali
huwa hawajavaa kofia ya kujikinga (helmet)
na ni wazi kabisa kwamba karibia wote huwa hawana kofia hiyo kwa mteja wao.
Isionekane tena kawaida abiria wa bodaboda kutokua na kofia, sheria kali
zinahitajika sambamba na ufuatiliaji wa karibu. Wengine hubeba abiria zaidi ya
mmoja (wenyewe wanaita mshikaki). Madereva wengine wa bodaboda huendesha wakiwa
wamelewa pombe ama madawa mengine ya kulevya, kile kipimo cha pombe cha
kupuliza kisiishie tu kwa wenye magari bali hata kwa hawa wa pikipiki maana
ndio wanaosababisha ajali nyingi zaidi. Japo sijawahi kutana na chuo cha
udereva wa bodaboda ila nadhani kungekuwa na mafunzo flani ambayo mtu anapitia
kabla ya kuwa dereva wa bodaboda ingewasaidia kujifunza sheria za barabarani
maana kwa kilichonitokea mimi hapo juu inaonesha wazi weledi wa yule dereva
(labda kipo ila mimi sijui).
Pia tunaweza kupunguza kiasi cha athari pindi ajali
zinapotokea. Kitu muhimu kuliko vyote kwa mtu aliyepata ajali ni huduma
anayoipata kabla ya kufikishwa hospitali japo wengi huwa tunataka kumkimbiza
hospitali kabla ya yote. Mara nyingi askari ndio wanahusika pale ajali
inapotokea, kwa bahati mbaya inaonekana mafunzo yao hayahusishi kutoa huduma ya
kwanza kwa mtu aliyepata ajali. Kuingiza mafunzo kama hayo sambamba na yale ya
uaskari inaweza kupunguza namba ya watu wanaokufa kwa ajali ama athari
zinazoweza kujitokeza. Pia, watu wanaokuja kusaidia baada ya ajali huwa ni
wasamalia wema ambao nao huwa hawana ujuzi wa nini cha kufanya zaidi ya
kuwapepea na kuwawahisha hospitali majeruhi; kuingiza mafunzo mashuleni ya nini
cha kufanya mtu unapofika kuwasaidia majeruhi huenda ikawa ni njia sahihi ya
kupunguza athari za ajali hizi kwa msaada kutoka kwa wasamalia wema.
Nimalize kwa kusema pindi ukijikuta unataka kuchagua chombo
gani cha kupanda mbele ya vilivyopo machoni mwako kwa ajili ya usafiri, basi
zingatia haya.
Japo mafunzo yatatolewa kwa bodaboda,askari na hata kwa wananchi kwa njia ulizozipendekeza,fikra na hulka ya watanzania isipokubali kubadilika mambo haya ya ajali hayataisha.
ReplyDeleteUkweli ni kuwa watu wote twajua kwamba mwendo kasi na kutokuzifuata hzo sheria za barabara ndizo zaleta yote haya madhara,lakini twazifata? Hapana ndo jibu,Tubadilike.
Ni kweli kubadili tabia ina ugumu wake ila inaweza kuharakishwa na usimamizi mkali wa sheria
Delete