Saturday, 24 September 2016

TIBA MBADALA: FUNDISHO LA LOLIONDO HALIKUELEWEKA



TIBA MBADALA: FUNDISHO LA LOLIONDO HALIKUELEWEKA
Nusu ya kwanza ya mwaka 2010 inakumbukwa hapa kwetu kwa habari ya “kikombe cha babu” nadhani kuliko vitu vyote vilivyotokea kipindi hicho. Habari zilitapakaa ndani na nje ya nchi kwamba huko nyikani katika kijiji cha Samunge, Loliondo mkoani Arusha ametokea mzee ambaye ni mchungaji mstaafu wa kanisa la KKKT, aliyestaafu tangu mwaka 2002 anayetoa dawa ya mti-shamba inayotibu magonjwa yote. Ulichotakiwa kufanya ni kwenda kule aliko na anakotengenezea dawa hiyo na kunywa kikombe palepale kwa shilingi 500/- tu  na utakuwa umepona ugonjwa wako, haijalishi ni kifafa, kisukari, shinikizo la damu, pumu, saratani, UKIMWI ama ugonjwa wowote ule. Samunge kulijaa watu, kulikuwa na foleni ndefu ya magari iliyokwenda mpaka km 50 na babu alisema kulipojaa watu alitoa vikombe 17,000 kwa siku. Kulikuwa na taarifa za watu kuondoka mahospitalini kukimbilia kikombe, wengine kuacha dawa zao baada ya kunywa kikombe, na inasemekana hata watumishi kwenye tiba  ya kisasa nao walikwenda kupata kikombe. Wengine hawakufanikiwa kupata kikombe kwani walipoteza maisha wakiwa  kwenye foleni na kuzikwa kulekule. Wanasiasa nao walikwenda kupata kikombe, wengine walikunywa mbele ya kamera na kutoa ushuhuda kwamba wamepona(bila kufanya vpimo lakini).
 Image result for babu wa loliondo
Aliyeachwa yatima tangu akiwa mdogo, hakuwa na elimu nyingine isipokuwa ile ya “bible skuli”, Ambilikila Mwasapila maarufu kama babu wa Loliondo aliyekuwa na umri wa miaka 74 wakati anapata umaarufu inaonesha alikuwa mtu wa kuamini na kufuata kile ubongo wake ulichofanya wakati amelala usingizi(ndoto). Kwani alipokuwa kijana alipata vishawishi vya kutaka kuachana na mambo ya kanisa na kwenda kuchimba madini ila aliota ndoto kwamba anashika madini na mikono yake inaunguzwa na madini yale, akajua hakutakiwa kwenda kuchimba madini. Kwenye mahojiano aliyoyafanya na Mika Vähäkangas babu anasema kila aliposali jioni na kuomba kitu basi alipata majibu haraka kwenye ndoto. Mnamo Januari mwaka 1991 babu aliota ndoto nyingine ambamo alimuona mwanamke asiyemfahamu na alisikia sauti ya Mungu ikimwambia “mpe ile dawa yako na ataponywa UKIMWI”. Mwaka 2009 akiwa amekaa kanisani akisubiri mazoezi ya kwaya babu alimuona yule mwanamke mwenye UKIMWI aliyemuota miaka 18 iliyopita. Usiku wake babu aliota mtu akimpa mizizi miwili mmoja kila mkono na jinsi ya kuandaa dawa na hapo ndipo alipopata majibu kwamba mizizi ile ndiyo dawa anazotakiwa kumpa yuele mwanamke(yule mwanamke aliitwa Mama Upendo). Mika Vähäkangas alipomuhoji Mama Upendo alimwambia kwamba baada ya kutumia dawa ya babu alijiona amepona UKIMWI na alitupa dawa zake za ARV, alipokwenda kupima anasema madaktari walimwambia hawaoni virusi vya HIV kwenye damu yake. Nashindwa kuelewa kwanini Mika Vähäkangas hakuomba aoneshwe majibu hayo ya hospitali na hatuna uthibbitisho kama kweli mama huyu alikuwa ameambukizwa HIV na alikua anapata matibabu katika kituo fulani. Hiyo ilikuwa mwezi wa tano mwaka 2009 na tangu hapo habari za babu zikaanza kusambaa kwa njia ya ushuhuda wa mdomo na watu wao wenyewe kupona na wengine wengi wakamiminika huko.

Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ilionesha kwamba majaribio yaliyofanywa kwa panya(ila sio kwa binadamu) yanaonesha mti huo wa babu ambao wataalamu wa sayansi ya mimea wanautambua kwa jina la Carissa spinarum(mwanzoni uliitwa Carissa edulis) unaweza kuondoa degedege, kupunguza sukari kwenye damu, kupunguza shinikizo la damu, kukinga magonjwa ya ini, na kuua virusi aina ya Herpes Simplex(HSV) vyote hivyo kwenye panya wa majaribio. Mti huu ujulikanao kama “mugariga” wamaasai huuita “Engamuriaki” ama “Olmuriaki” na wasonjo huuita “Engamuriaga” ulikuepo hata kabla ya babu kuwepo na wamaasai na wasonjo waliutumia kuchanganya na maziwa ama nyama, makabila mengine hapa kwetu yanayotumia mmea huu kwenye vyakula ni wakurya, wagogo, na wabarbaig. Mmea huu pia haupatikani Tanzania pekee bali upo pia katika nchi za Australia, Botswana, Cambodia, Cameroon, Eritrea, Ethiopia, Ghana, Guinea, Japan, Kenya, Myanmar, Namibia, Nigeria, Papua, Saudi Arabia, Senegal, South Africa, Sudan, Thailand, Uganda, Vietnam na Yemen. Hatupo peke yetu. Mti huu pia hutumika kama dawa nyingine za mitishamba hapa Tanzania na huko kwingine hata kabla ya babu kuanza kuutumia, matumizi yake hujumuisha tiba dhidi ya kifafa, maumivu ya kichwa, matatizo ya kifua, gono, kaswende, na kichaa cha mbwa.

Kama ndoto isivyochukua muda mrefu pindi unapostuka kutoka usingizini, umaarufu wa Babu wa Loliondo nao haukuchukua muda mrefu. Habari za watu waliorudi kutoka kunywa kikombe wakagundua hawajapona na wale walioacha dawa za ARV walipoanza kupoteza maisha yao zilishika hatamu na kikombe cha babu kikapoteza kiki. Binafsi ndugu zangu wa karibu sana walikwenda kupata kikombe ila hakuna aliyepona.

Wakati babu anakuja na wazo la kuanza kutoa kikombe alikua amekwishastaafu na alikua anaishi kwa pension ya sh. 20,000/- kwa mwezi na pia akifanya kazi kama fundi muashi, aliishi kwenye kijumba cha tope alichopewa akae na rafiki yake na hakutaka kurudi Babati ilikokua familia yake. Gazeti la Daily Nation la tarehe 24/11/2012 lilimtembelea babu miaka miwili baada ya habari ya kikombe na kuona jinsi maisha yake yalivyobadilika. Kulikuwa na mashine ya unga moja tu kwenye kijiji hicho ambayo babu aliimiliki, Babu alikuwa anamiliki nyumba mpya ya tofali iliyoezekwa bati, yenye choo na bafu kwa ndani na ilikuwa ina vyumba vitatu vya kulala, solar kwa ajili ya umeme, dishi la satellite alilotumia kwa ajili ya TV yake na babu pia alikuwa na bomba la maji nyumbani kwake. Kwenye uwanja wake lilipaki roli la tani 14 alilonunua kwa shilingi milioni 14 na Toyota Land Cruser aliyonunua kwa shilingi milioni 60, pia babu alikuwa ameajiri wafanyakazi 31 aliowalipa wastani wa shilingi 150,000/- kwa mwezi kila mmoja. Ni dhahiri kwamba kikombe kilibadilisha maisha ya babu. Huenda alivutwa na tamaa ya hivi vitu hata akajikuta anakuwa mganga wa kienyeji?sina uhakika, ninawaza tu.

Kwa kuwa Mugariga ni mmea uliokuwepo vizazi na vizazi kabla ya Babu wa Loliondo, naamini kikubwa kilichowavuta watu kwenda Samunge ni ndoto za babu. Huenda babu alikuwa mtu mwaminifu aliyemtumikia Mungu wake na kweli alikuwa akiyaota hayo aliyoyadai. Sijui kuhusu kuota uso wa mwanadamu ambae hujawahi kumuona kabla(labda wana saikolojia wanajua zaidi) ila tunaambiwa tunakumbuka 5%  pekee ya ndoto tunazopata tukiwa tumelala. Wafaransa wana neno “Déjà vu” ambalo linamaanisha unahisi kwa uhakika kabisa kwamba ulishawahi kuona kitu fulani huko nyuma ambacho unakiona sasa ila ukweli ni kwamba hujawahi, wengi inatutokea hii, huenda babu nae alikuwa na Déjà vu tu. Ubongo wetu wanadamu uaweza kutuchezea na kutudanganya jinsi dunia ilivyo, kwa mfano ubongo wako hapo ulipo unakwambia dunia imesimama na pia jua linatembea kutoka mashariki kwenda magharibi lakini ukweli ni kwamba dunia inakimbia katika mwendo wa 108,000 km/hr ikizunguka jua na jua halitembei ila limesimama. Njia za kisayansi na ujuzi wa hesabu za uwezekano vinaweza kutuambia kile ambacho ubongo wetu unatudandanya. Tukija kwenye mambo ya kuota ndoto na kukutana na hicho tulichokiota baadae hebu tujiulize ni mara ngapi pia tumeota kitu na kisitokee(lazima tu ni mara nyingi zaidi) ila ubongo wetu unapenda kukumbuka wakati ule kimetokea na kupotezea yale mengi ambayo hayakutokea. Binafsi nimewahi kuota ajali ya ndege na kesho yake nikasikia habari kuwa ndege imeanguka ziwa Victoria, ila nimewahi kuota ajali nyingine nyingi ambazo hazikuwahi kutokea pia na kwaiyo sina haja ya kujiona nina upekee fulani bali ilitokea tu. Kwa jinsi ilivyokuwa gharama kwenda kwa Babu wa Loliondo ukilinganisha na kwenda hospitalini, inaonesha sisi tulivyo wagumu wa kuwekeza katika afya ya kweli na ndio maana wakina Juma Mwaka na wenzie walizidi kushika hatamu na njia zao mbovu zisizofuata utaratibu. Kuweka maisha yetu mikononi mwa mtu aliyeota dawa ilionesha ufinyu wa mbinu zetu za uchambuzi wa matukio kwa kutumia hesabu za uwezekano na mbinu za kisayansi.

Kinachoendelea nchini na hawa wanaojiita wanafanya Tiba Mbadala bila ya kufuata utaratibu inaonesha somo la kikombe cha babu halikutuingia vyema. Watu hawa wana nguvu na ushawishi na wana wateja wengi kiasi cha kupinga maagizo ya serikali katika mahakama kuu. Watu hawa watasimama kwenye runinga na kutuambia wana dawa ya ugonjwa fulani sugu na watu kadhaa imewaponya na sisi tutawakimbilia kama tulivyomkimbilia Babu wa Loliondo. Binafsi sikatai kwamba huenda kukawa na mitishamba ambayo inatibu magonjwa kwani hata madawa kama Quinine na mengine yametokana na mimea ila njia zinazotumika kuwafanya watu watumie hizo dawa sio sahihi, mfano kuota pekee. Labda serikali inavyowataka wanafunzi wote kuchukua masomo ya sayansi tutabadilika japo sidhani sana.

5 comments:

  1. Watu wanafuata huduma nzuri muda mwingine . yan ile sense of being cared . huku kwetu unakuta vitu vipo tu ila ile customer care inakuwa haipo so as human nature kila mtu anapenda kuwa cared kuthaminiwa n.k sometimes hii inafanya biashara hii kukua sana Na kuwa maarufu .

    ReplyDelete
    Replies
    1. Yeah kweli,
      Inabidi tujifunze na sisi kuongeza care ila kumbuka wao wana wateja wachache wanye uwezo mkubwa kifedha

      Delete
  2. Nitangulize hongera zangu kwa mwandishi wa makala hii Joseph J. Masalu kwa kutoa muda wake kuweza kuongelea mambo mbalimbali hususani yale yanayogusa sekta ya afya ambayo inamgusa kila mmoja wetu.
    Ni takribani miongo mitano sasa tangu nchi yetu ipate uhuru kutoka kwa wakoloni. Mwanzoni mwa 1960 Huduma za afya zilikuwa duni na ngumu kupatikana hivyo kufanya watu wengi kuendelea na kuamini tiba zetu za asili ambazo wamekuwa wakitumia, na imeendelea hivyo miaka nenda rudi ingawa teknologia inakua na kufanya utafiti na matibabu kuwa ya kisayansi zaidi.
    Nachotaka kuonesha ni kwamba bado tuna imani kubwa sana na tiba mbadala.
    Tunachotakiwa kufanya ni kuwekeza zaidi kwenye afya ili kuboresha huduma zetu za afya hii itafanya watu kuamini na kutumia hospitali badala ya tiba mbadala.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Unaweza kusoma makala nyingine inayofanana na hii kwa kubofya http://medstuinfo.blogspot.com/2015/10/tiba-iliyotukuka-tiba-ya-kisasa-na.html?m=1

      Delete