Wengi tunafahamu kuwa uzito uliopitiliza sio kitu kizuri
kiafya. Huweza kutuongezea uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya
kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu, kiharusi, saratani za
aina mbalimbali na kadhalika. Shirika la afya duniani (WHO) linakadiria kuwa
mwaka 2014 kulikuwa na watu zaidi ya bilioni 1.9 waliokuwa na uzito uliozidi
kiwango. Tunaweza kujua endapo uzito tulio nao ndio unaotakiwa ama umezidi kwa
kuchukua uzito wetu katika kilogramu na kisha kuugawanya kwa kipeo cha pili cha
urefu wetu katika mita (kurahisisha: chukua uzito wako katika kilogramu;chukua
urefu wako katika mita; uzito wako gawia urefu wako; jibu ulilopata gawia tena
urefu wako). Jibu likizidi 25 basi wewe uzito wako upo juu ya kiwango
kinachotakiwa na unatakiwa kuanza jitihada za kuupunguza ili kupata afya njema.

Kwa kuwa jamii imeelimika juu ya madhara ya uzito uliozidi
kiwango na kunuia kuupunguza basi wamejitokeza watu mbalimbali wanaotaka
kusaidia kwa hilo, baadhi yao wapo sahihi kwa kufuata njia zilizothibitishwa
kisayansi kwa kufanyiwa utafiti, na wapo ambao hawako sahihi aidha wakiwa na
lengo la kuuza bidhaa zao za uwongo ama wameshindwa tu kung’amua sayansi ya
nishati na chakula.
Kinachotufanya kunenepa ni kuongezeka kwa kiasi cha mafuta
tunachotunza mwilini mwetu pale ambapo tumekula chakula kingi zaidi ya kile
miili yetu inachohitaji kwa matumizi yake. Kizazi chetu hiki kina chakula kingi
zaidi (kinacholiwa kutokana na matabaka ya kiuchumi) na kimepunguza zaidi kazi
za kutumia nguvu na kuongeza shughuli zinazotufanya kukaa kwa muda mrefu kama
vile runinga, simu zenye intaneti, michezo ya kielektroniki na kadhalika. Kwa
kifupi ni kwamba tunanenepa pale tunapoingiza zaidi ya kutoa. Kama unafikiria
vizuri utakua umekwishaona kwamba ili upunguze uzito inabidi uende kinyume na
sababu iliyokufanya unenepe, yaani utoe kiasi kinachozidi.
Blog ya Afya na Kiasi inamnukuu Juma Mwaka akisema kwamba
kutumia juice za matango, karoti na nyanya kila siku kwa muda wa mwezi mmoja
ndio njia ya kupunguza kitambi. Hii si kweli kwani ukifanya hivi na wakati
hufanyi mazoezi wala kupunguza kula vyakula vyenye nishati kwa wingi kitambi
chako kitabaki palepale ama kuongezeka. Nisimlaumu sana Mwaka kwani anaonekana
hata haufahamu vyema mfumo wa chakula kwani anasema “mtu anapokula chakula ni
lazima kwanza kiishe kingine, vinginevyo anakuwa ametunza sumu mwilini kutokana
na kuwa na mabaki mengi ya chakula cha takribani hata mwaka mmoja” na
anathibitisha kwa kusema “binadamu hufa akikosa chakula kwa siku nyingi”, yeye
anadhani tumbo ni kama pipa la kutunzia chakula na hajui hata mwili unatunza
vipi chakula ili utumie pale unapokosa. Ukweli ni kwamba yakipita masaa manne
hadi matano baada ya kula basi takribani chakula chote kinakuwa kimeondoka
tumboni mwako; na pia mwili hutunza chakula kinachozidi kwanza katika ini na
kingine katika hali ya mafuta, wakati ambapo hakuna chakula basi mwili huingia
katika stoo zake hizi na kumeng’enya. Mwaka pia anatuambia kunywa maji ya
uvuguvugu kutaondoa kitambi. Huu nao ni uwongo kwani maji ya moto hayachomi
mafuta na yakishaingia mwilini yanapozwa kufanana na joto la mwili tu.
Sikushangaa kusikia huyu Mwaka amefutiwa usajiri.
Mwingine anaitwa Dr. Boaz Mkumbo kwenye blog yake ya doctorboaz.blogspot.com.
Huyu ameandika kuwa amesomea udaktari wa binadamu katika chuo cha Bugando na
inaonekana anachanganya tiba mbadala na ya kisasa (sina neno nae kama ni ya
kweli anayofanya). Moja ya huduma anayotoa ni kusafisha utumbo mpana, yaani
wanaingiza kimiminika (mfano: kahawa) kwenye utumbo mpana kupitia njia ya haja
kubwa. Anasema tiba hiyo inapunguza unene, kuondoa sumu(Makala yangu huko nyuma
ilikataa mambo ya sumu) na kutibu magonjwa mengine. Kwanza tu labda nimwambie
kwamba kuta za utumbo mpana ni safi na haziitaji kusafishwa, binafsi nimewahi
kuzichungulia kwa mgonjwa aliekuwa anachunguzwa utumbo mpana kwa kamera
inayoingizwa kwa mpira kupitia sehemu ya haja kubwa; na kuhusu unene:
kimiminika kinachoingizwa kwenye utumbo mpana huwa kina tabia ya kufyonza maji
kutoka kwenye utumbo mpana na kumfanya mtu aharishe; mtu akiharisha basi
apoteza maji mengi mwilini na hivyo atapungua uzito ila baada ya siku kadhaa
mwili wake utapata maji na uzito wake utarudi palepale. Lakini njia hii yaweza
kuwa na madhara kwa afya pia kwani mtu anaweza kuharisha kupita kiasi, anaweza
kuambukizwa magonjwa kama amoeba ama homa ya ini kama watachangia vifaa,
anaweza kutobolewa utumbo mpana wake na kadhalika, kwa hiyo si salama.
Mtandao mmojawapo ambamo waweza pata taarifa sahihi za
kuhusu kupunguza uzito ni www.jamiihealthtz.com.
Nimalizie kwa kushauri kwamba ukisikia njia ya kupunguza uzito ambayo haihitaji
jitihada, nguvu, yenye kukaa tu chini, uwezekano ni mkubwa njia hiyo ikawa ni
ya uwongo.
Nmeelewa sana daktari
ReplyDeleteKaribu sana
ReplyDeleteUkitaka kupunguza kitambi kwa siku moja kafanye Liposuction kama hyo pesa unayo.
DeleteGreat stuff
ReplyDelete