UPOTOSHAJI: TOFAUTI
ZA KIAKILI KATI YA MATAIFA
Miezi kadhaa iliyopita kulikua na video inasambaa kwenye
mitandao ya kijamii ambapo alionekana mwanasaikolojia mkanada, marehemu John
Phillipe Rushton akielezea kuhusu tofauti za kipimo cha akili (IQ) kati ya
wazungu, watu wa Asia na waafrika. Inaonekana alikua amearikwa kulisemea hilo
kwenye mkutano wa kikundi kinachojiita “American Renaissance”. Baada ya hapo
ilinibidi niingie kwenye website yao ya http://www.amren.com/ ambapo baada ya kuperuzi kidogo
nikagundua hawa ni watu wabaguzi wa rangi ambao mawazo yao bado yameganda zaidi
ya karne moja kurudi nyuma. Ukiingia kwenye website yao unakaribishwa na maneno
ambayo yanamaanisha: wao wanapinga mawazo ya kusema kwamba watu wa rangi zote
ni sawa;wanaandika kwamba Marekani sio sehemu ambapo mtu yeyote anaweza kwenda kuchukua
tu vitu, na sio sehemu ambapo kila mtu anaetaka kwenda anaenda,ni sehemu ambayo
ilianzishwa na wazungu. Hayo ni baadhi tu ukiachilia mbali kwamba wanamuunga
mkono kutoka moyoni mwanasiasa Donald Trump.
Basi nimeona ni vyema leo tukaliangalia hili swala la uwezo
wa kiakili kama unavyopimwa na IQ. Tuone kama mengi wanayodai hawa watu yana
ukweli ndani yake. Tutaangalia maana ya IQ, tutachimbua kuona pia kama kuna
utofauti wa IQ kati ya mataifa na tutajaribu kuona kama ni hivyo sababu ni zipi
na je hali yaweza kubadilika ama la. Lakini kabla ya kwenda mbali ni vyema
tukajua kwamba kwenye maswala yanayohusu akili hata wataalamu na wasomi wa hii
fani bado wanabishana sana kuhusu mambo mengi, hakuna mengi yanayojulikana
bayana; kwa hiyo lazima tuwashangae watu wanaokuja mbele kwa kujiamini na
kusema vitu kana kwamba vimethibitishwa
wakati wao wenyewe wakijua kabisa kuna ubishani bado, ndio maana wengine
wanapata hisia kwamba watu hawa wana ajenda nyingine binafsi.
IQ ni kifupi cha neno la kiingereza Intelligence Quotient . IQ hupima uwezo wa akili. Profesa wa
Saikolojia wa chuo kikuu cha Delaware, Linda Gottfredson anafafanua akili kama
uwezo wa kuchambua, kupanga, kutatua matatizo, kufikiria kwa undani, kuelewa
vitu vigumu, kujifunza kwa uharaka na kujifunza kutokana na ya uzoefu. Na sio
tu usomaji vitabu, kijiutaalamu fulani cha kitaaluma au ufauru katika majaribio
darasani pekee. Badala yake inaakisi kwa kina na mapana uwezo wa kuyaelewa
yanayotuzunguka. Kuna aina ambili za akili. Ya kwanza inahusu ufahamu alionao
mtu kuhusu jinsi dunia ilivyo na mambo aliyojifunza ambayo humsaidia kutatua
matatizo, waingereza wanaiita crystallised
intelligence. Ya pili inahusu uwezo wa kutatua matatizo mapya ambayo inahusiana
kwa kiasi kidogo na taarifa alizo nazo mtu ama uwezo wake wa kujifunza,
waiingereza wanaiita fluid intelligence.
Kuna majaribio mbalimbali yanayotumika kupima IQ ya mtu.
Mambo haya ya utofauti wa kiakili kati ya mataifa yaliletwa
kwenye hadhira mnamo mwaka 1994 baada ya Richard Herrnstein na Charles Murray
kuchapisha kitabu chao kilichoitwa The
Bell Curve. Kitabu hicho kilisema kwamba: IQ ni utabiri wa mafanikio ya mtu
ya baadae, kwamba utofauti wa IQ kati ya mataifa ni wa kurithi na mazingira
hayahusiki kabisa na utofauti huo na elimu ina nafasi ndogo sana katika swala
la IQ. Kitabu hicho kilikua maarufu na kiliuza zaidi ya nakala 300,000. Baada
ya hayo, umoja wa wanasaikolojia wa Mrekani (APA) waliunda kikundi cha wabobezi
wa mambo ya akili wakiongozwa na Ulrich Neisser na wakatoa chapisho lao ambalo
kwa kiasi kikubwa lilipinga kitabu hicho. Mengi ninayoandika hapa walikubaliana
kikundi hicho cha wanasaikolojia waliobobea katika maswala ya akili.
Kabla ya kufika mbali ni vyema tukajua kuna milengo mikuu
miwili kwa wanasaikolojia kuhusu haya mambo ya IQ; mlengo mmoja ni ule unaoona
kua tofauti za IQ ni za kurithi na mwingine unaoona kua sababu ni mazingira kwa
kiasi kikubwa. Kuhusu utofauti wa IQ kati ya mataifa, tafiti za mwanzo
zilionesha kwamba watu wa Asia Mashariki wana wastani wa IQ ya 106, wazungu
100, watu weusi waishio marekani 85 na watu weusi waishio kusini mwa jangwa la
Sahara 70. Kuhusu hili, Umoja wa Wanasaikolojia wa Marekani nawanukuu wakisema “Hakuna vithibitisho vya kutosha vya moja
kwa moja kuhusu hili, lakini hata vile vichache vilivyopo vimeshindwa kuunga
mkono mlengo wa kurithi”
Moja kati ya tafiti za muhimu kabisa katika kuonesha kua tofauti
za IQ si za kurithi ni zile zilizofanyika kwa watoto waliochukuliwa kulelewa na
wazazi ambao sio wao, hawa hawajarithi chochote kwa walezi wao, chochote
watakachokipata kutoka kwa walezi wao ni cha kujifunza na kinahusiana na
mazingira wanamolelewa. Moja ya tafiti ya aina hii iliwahi kufanywa mwaka 1986 na
mwanasaikojia Moore. Moore alichukua watoto wenye wastani wa umri wa miaka minane
na nusu ambao aidha walikua wamezaliwa na wazazi weusi ama mchanganyiko wa
wazazi weusi na weupe. Watoto hawa walikua wamechukuliwa kulelewa na wazazi
aidha weusi ama weupe ambao walikua wana kipato cha kati. Baada ya kuwafanyia
majaribio ya IQ, watoto ambao walikua ni machotara walionekana kuwa na IQ sawa
tu na wale weusi; hii inaonesha vinasaba vya watu weupe havina mchango wowote
kwenye IQ kwani vingekua na mchango basi tungeona utofauti kwa sababu wale
machotara wana nusu ya vinasaba vyao kutoka kwa mzazi mmoja mweupe. Pia watoto
walio lelewa kwenye familia za walezi weupe bila kujalisha kwamba wao ni
machotara ama weusi waliwazidi wale walio lelewa kwenye familia za walezi weusi
IQ kwa kiasi cha 13; hii namba 13 ipo karibu na 15 ambayo ni tofauti ya IQ kati
ya wamerekani weupe na weusi, hii inaonesha utofauti wa IQ unaoonekana
unatokana na mazingira wanayokulia watu kwa kiasi kikubwa. Mazingira hayo ni
kama vile ukaribu na vitu vya kusoma kama magazeti ama vitabu, kupata elimu
bora, kuongea na watoto wakiwa wadogo, kuwapa moyo watoto, kuanza shule mapema,
n.k.
Kwamba watu wa Asia mashariki wanaonekana kua na IQ kubwa
Zaidi ya wazungu na waafrika ilitokana na wao kufauru sana mitihani ya kuingia
vyuoni nchini marekani maarufu kama Scholastic
Aplitude Test (SAT) na kujipatia kazi zinazohitaji taaluma ya juu kama
udaktari, uinjinia, uanasheria, uanasayansi, n.k. Tafiti nyingine zimeonesha
kwamba wakipewa majaribio ya IQ wanapata sawa tu na wale weupe ila ikija kwenye
SAT wanapata Zaidi. Wanasaikolojia wanafafanua sababu kua ni kutokana na jinsi
watu wale wanavyowekeza katika kutaka kufauru ile mitihani. Watu wa Asia mashariki
hufuata filosofia ya Conficius ambamo
huamini kwamba kua na akili ni zao tu la kua na bidii, basi huweka bidii sana
katika kujifunza na kufauru mitihani.
Tafiti zilizofanywa mwaka 1987 na mwanasaikolojia Flynn
zilionesha kwamba kuna mataifa ambamo IQ inaongezeka kadri mataifa yale
yanavyozidi kua ya kisasa. Uongezekaji huo umeoneshwa kua wa kiasi cha 3 kwa
kila miaka kumi. Pia kwenye nchi ambazo zilianza kua za kisasa tangu karne ya
19 kama vile nchi za ukanda wa Scandinavia IQ imeonekana kufika kileleni na
hata kuanza kupungua kidogo. Inatarajiwa kwamba mnamo mwishoni mwa karne hii ya
21, IQ kwenye nchi zilizoanza kua za kisasa miaka ya hivi karibuni kama zetu
hizi zitafikia IQ sawa na nchi mfano wa zile za ukanda wa skandinavia. Hii
inaonesha kwamba IQ hutegemea mazingira kwa kiasi kikubwa.
Kurithi kwa hapa ina maana ya kupokea tabia fulani kutoka kwa
wazazi wa kibaiolojia. Kurithi ndiko kunamsababisha ndege awe na mabawa ila
mbwa asiwe nayo, kunakusababisha wewe utembee na miguu miwili na nyani
atembelee mine, n.k. Karibia kila tabia ya mwanadam ina chembe za kurithi na za
kutokurithi, kwa hiyo hata akili nayo ina chembe ambazo mtu amerithi ila sio
kwa 100% kama wabaguzi wa rangi wanavyotaka iwe ili ionekane kwamba wenye IQ
ndogo basi haiwezi badilika milele. Tuchukue urefu wa wanadam kama mfano, 90%
ya urefu wetu ni wa kurithi na 10% iliyobaki hutegemea mazingira tuliyokulia (
hapa ni vitu kama vyakula, afya njema, tiba, hali za mimba, n.k). Hata kama mtu
wazazi wake wana urefu kumpita Hashim Thabiti, anapokulia sehemu ambamo
mazingira niliyoyataja yapo vibaya, kuna uwezekano asiwe mrefu kama walivyo
wazazi wake. Lakini mtu huyu na ufupi wake alioupata kutokana na mazingira duni
akija kupata watoto na wakati huo akiwa na mazingira mazuri basi tunategemea
watoto wake waliokulia kwenye mazingira mazuri watakua warefu. Hata hivyo
vinasaba vyote vya mwanadamu vilijulikana mwaka 2003 baada ya mpango wa
kutafuta vinasaba vyote vya mwanadamu ulioitwa Human Genome Project kukamilika huko Marekani, lakini hakuna sehemu
wameonesha kwenye vinasaba inayohusisha utofauti wa akili kati ya mataifa.
Nihitimishe kwa kusema kwamba akili huweza kubadilika
kutokana na mazingira mtu aliyomo. Vilevile sisi waafrika tuache kujiona kwamba
hatuna akili na tusimkuze sana mtu mweupe maana inawezekana kua kama yeye
kiakili au kumpita. Tafiti zilizofanywa na Steele na Aronson mwaka 1995
zilionesha kwamba watu kuitwa na kukubali kua wao wana uwezo mdogo wa akili pia
huwafanya kushindwa kufikiria barabara na kupata vizuri kwenye majaribio ya IQ.
Kitu kikubwa kabisa kilichooneshwa na tafiti kwamba chaweza kukuza IQ ni elimu
bora, vingine ni kama kukuza uwezo wa kukumbuka vitu na mazoezi hasa kwa wazee.
Haihitaji mtu kuambiwa kuboresha elimu katika nchi kwa ujumla kutasababisha
tuishi maisha ya kuridhisha zaidi kwa kutatua matatizo yetu.
Umejitahidi sana kuweka mambo bayana,nimependa kazi hii, jamii ilikua imefumbwa....
ReplyDeleteTupo pamoja mkuu
DeleteEnter your comment...kila jamii inayojitegemea inauwezo wakiakili kulingana na mazingira yao,pia huwezo wakutatua matatizo unaligana na matatizo yaliopo katika jamii husika....kwa mfano ikitokea njaa,jamii husika itajifunza kutunza chakula
ReplyDeleteachalia mbali na watu wenye uwezo watofauti katika jamii(genius minds) ambao wameweza kugundua vitu vya kipekee kama umeme,speed ya mwanga nk
Yeah,
DeleteNi kweli
Good observations
ReplyDeleteGood observations
ReplyDeleteNice work Joseph Masalu
ReplyDeleteThank you
Delete