Saturday, 3 September 2016

UPOTOSHAJI: TOFAUTI ZA KIAKILI KATI YA MATAIFA



UPOTOSHAJI: TOFAUTI ZA KIAKILI KATI YA MATAIFA
Miezi kadhaa iliyopita kulikua na video inasambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo alionekana mwanasaikolojia mkanada, marehemu John Phillipe Rushton akielezea kuhusu tofauti za kipimo cha akili (IQ) kati ya wazungu, watu wa Asia na waafrika. Inaonekana alikua amearikwa kulisemea hilo kwenye mkutano wa kikundi kinachojiita “American Renaissance”. Baada ya hapo ilinibidi niingie kwenye website yao ya http://www.amren.com/ ambapo baada ya kuperuzi kidogo nikagundua hawa ni watu wabaguzi wa rangi ambao mawazo yao bado yameganda zaidi ya karne moja kurudi nyuma. Ukiingia kwenye website yao unakaribishwa na maneno ambayo yanamaanisha: wao wanapinga mawazo ya kusema kwamba watu wa rangi zote ni sawa;wanaandika kwamba Marekani sio sehemu ambapo mtu yeyote anaweza kwenda kuchukua tu vitu, na sio sehemu ambapo kila mtu anaetaka kwenda anaenda,ni sehemu ambayo ilianzishwa na wazungu. Hayo ni baadhi tu ukiachilia mbali kwamba wanamuunga mkono kutoka moyoni mwanasiasa Donald Trump.

Basi nimeona ni vyema leo tukaliangalia hili swala la uwezo wa kiakili kama unavyopimwa na IQ. Tuone kama mengi wanayodai hawa watu yana ukweli ndani yake. Tutaangalia maana ya IQ, tutachimbua kuona pia kama kuna utofauti wa IQ kati ya mataifa na tutajaribu kuona kama ni hivyo sababu ni zipi na je hali yaweza kubadilika ama la. Lakini kabla ya kwenda mbali ni vyema tukajua kwamba kwenye maswala yanayohusu akili hata wataalamu na wasomi wa hii fani bado wanabishana sana kuhusu mambo mengi, hakuna mengi yanayojulikana bayana; kwa hiyo lazima tuwashangae watu wanaokuja mbele kwa kujiamini na kusema vitu kana kwamba vimethibitishwa  wakati wao wenyewe wakijua kabisa kuna ubishani bado, ndio maana wengine wanapata hisia kwamba watu hawa wana ajenda nyingine binafsi. 

   

IQ ni kifupi cha neno la kiingereza Intelligence Quotient . IQ hupima uwezo wa akili. Profesa wa Saikolojia wa chuo kikuu cha Delaware, Linda Gottfredson anafafanua akili kama uwezo wa kuchambua, kupanga, kutatua matatizo, kufikiria kwa undani, kuelewa vitu vigumu, kujifunza kwa uharaka na kujifunza kutokana na ya uzoefu. Na sio tu usomaji vitabu, kijiutaalamu fulani cha kitaaluma au ufauru katika majaribio darasani pekee. Badala yake inaakisi kwa kina na mapana uwezo wa kuyaelewa yanayotuzunguka. Kuna aina ambili za akili. Ya kwanza inahusu ufahamu alionao mtu kuhusu jinsi dunia ilivyo na mambo aliyojifunza ambayo humsaidia kutatua matatizo, waingereza wanaiita crystallised intelligence. Ya pili inahusu uwezo wa kutatua matatizo mapya ambayo inahusiana kwa kiasi kidogo na taarifa alizo nazo mtu ama uwezo wake wa kujifunza, waiingereza wanaiita fluid intelligence. Kuna majaribio mbalimbali yanayotumika kupima IQ ya mtu.

Mambo haya ya utofauti wa kiakili kati ya mataifa yaliletwa kwenye hadhira mnamo mwaka 1994 baada ya Richard Herrnstein na Charles Murray kuchapisha kitabu chao kilichoitwa The Bell Curve. Kitabu hicho kilisema kwamba: IQ ni utabiri wa mafanikio ya mtu ya baadae, kwamba utofauti wa IQ kati ya mataifa ni wa kurithi na mazingira hayahusiki kabisa na utofauti huo na elimu ina nafasi ndogo sana katika swala la IQ. Kitabu hicho kilikua maarufu na kiliuza zaidi ya nakala 300,000. Baada ya hayo, umoja wa wanasaikolojia wa Mrekani (APA) waliunda kikundi cha wabobezi wa mambo ya akili wakiongozwa na Ulrich Neisser na wakatoa chapisho lao ambalo kwa kiasi kikubwa lilipinga kitabu hicho. Mengi ninayoandika hapa walikubaliana kikundi hicho cha wanasaikolojia waliobobea katika maswala ya akili.

Kabla ya kufika mbali ni vyema tukajua kuna milengo mikuu miwili kwa wanasaikolojia kuhusu haya mambo ya IQ; mlengo mmoja ni ule unaoona kua tofauti za IQ ni za kurithi na mwingine unaoona kua sababu ni mazingira kwa kiasi kikubwa. Kuhusu utofauti wa IQ kati ya mataifa, tafiti za mwanzo zilionesha kwamba watu wa Asia Mashariki wana wastani wa IQ ya 106, wazungu 100, watu weusi waishio marekani 85 na watu weusi waishio kusini mwa jangwa la Sahara 70. Kuhusu hili, Umoja wa Wanasaikolojia wa Marekani nawanukuu wakisema “Hakuna vithibitisho vya kutosha vya moja kwa moja kuhusu hili, lakini hata vile vichache vilivyopo vimeshindwa kuunga mkono mlengo wa kurithi”

Moja kati ya tafiti za muhimu kabisa katika kuonesha kua tofauti za IQ si za kurithi ni zile zilizofanyika kwa watoto waliochukuliwa kulelewa na wazazi ambao sio wao, hawa hawajarithi chochote kwa walezi wao, chochote watakachokipata kutoka kwa walezi wao ni cha kujifunza na kinahusiana na mazingira wanamolelewa. Moja ya tafiti ya aina hii iliwahi kufanywa mwaka 1986 na mwanasaikojia Moore. Moore alichukua watoto wenye wastani wa umri wa miaka minane na nusu ambao aidha walikua wamezaliwa na wazazi weusi ama mchanganyiko wa wazazi weusi na weupe. Watoto hawa walikua wamechukuliwa kulelewa na wazazi aidha weusi ama weupe ambao walikua wana kipato cha kati. Baada ya kuwafanyia majaribio ya IQ, watoto ambao walikua ni machotara walionekana kuwa na IQ sawa tu na wale weusi; hii inaonesha vinasaba vya watu weupe havina mchango wowote kwenye IQ kwani vingekua na mchango basi tungeona utofauti kwa sababu wale machotara wana nusu ya vinasaba vyao kutoka kwa mzazi mmoja mweupe. Pia watoto walio lelewa kwenye familia za walezi weupe bila kujalisha kwamba wao ni machotara ama weusi waliwazidi wale walio lelewa kwenye familia za walezi weusi IQ kwa kiasi cha 13; hii namba 13 ipo karibu na 15 ambayo ni tofauti ya IQ kati ya wamerekani weupe na weusi, hii inaonesha utofauti wa IQ unaoonekana unatokana na mazingira wanayokulia watu kwa kiasi kikubwa. Mazingira hayo ni kama vile ukaribu na vitu vya kusoma kama magazeti ama vitabu, kupata elimu bora, kuongea na watoto wakiwa wadogo, kuwapa moyo watoto, kuanza shule mapema, n.k.

Kwamba watu wa Asia mashariki wanaonekana kua na IQ kubwa Zaidi ya wazungu na waafrika ilitokana na wao kufauru sana mitihani ya kuingia vyuoni nchini marekani maarufu kama Scholastic Aplitude Test (SAT) na kujipatia kazi zinazohitaji taaluma ya juu kama udaktari, uinjinia, uanasheria, uanasayansi, n.k. Tafiti nyingine zimeonesha kwamba wakipewa majaribio ya IQ wanapata sawa tu na wale weupe ila ikija kwenye SAT wanapata Zaidi. Wanasaikolojia wanafafanua sababu kua ni kutokana na jinsi watu wale wanavyowekeza katika kutaka kufauru ile mitihani. Watu wa Asia mashariki hufuata filosofia ya Conficius ambamo huamini kwamba kua na akili ni zao tu la kua na bidii, basi huweka bidii sana katika kujifunza na kufauru mitihani.

Tafiti zilizofanywa mwaka 1987 na mwanasaikolojia Flynn zilionesha kwamba kuna mataifa ambamo IQ inaongezeka kadri mataifa yale yanavyozidi kua ya kisasa. Uongezekaji huo umeoneshwa kua wa kiasi cha 3 kwa kila miaka kumi. Pia kwenye nchi ambazo zilianza kua za kisasa tangu karne ya 19 kama vile nchi za ukanda wa Scandinavia IQ imeonekana kufika kileleni na hata kuanza kupungua kidogo. Inatarajiwa kwamba mnamo mwishoni mwa karne hii ya 21, IQ kwenye nchi zilizoanza kua za kisasa miaka ya hivi karibuni kama zetu hizi zitafikia IQ sawa na nchi mfano wa zile za ukanda wa skandinavia. Hii inaonesha kwamba IQ hutegemea mazingira kwa kiasi kikubwa.

Kurithi kwa hapa ina maana ya kupokea tabia fulani kutoka kwa wazazi wa kibaiolojia. Kurithi ndiko kunamsababisha ndege awe na mabawa ila mbwa asiwe nayo, kunakusababisha wewe utembee na miguu miwili na nyani atembelee mine, n.k. Karibia kila tabia ya mwanadam ina chembe za kurithi na za kutokurithi, kwa hiyo hata akili nayo ina chembe ambazo mtu amerithi ila sio kwa 100% kama wabaguzi wa rangi wanavyotaka iwe ili ionekane kwamba wenye IQ ndogo basi haiwezi badilika milele. Tuchukue urefu wa wanadam kama mfano, 90% ya urefu wetu ni wa kurithi na 10% iliyobaki hutegemea mazingira tuliyokulia ( hapa ni vitu kama vyakula, afya njema, tiba, hali za mimba, n.k). Hata kama mtu wazazi wake wana urefu kumpita Hashim Thabiti, anapokulia sehemu ambamo mazingira niliyoyataja yapo vibaya, kuna uwezekano asiwe mrefu kama walivyo wazazi wake. Lakini mtu huyu na ufupi wake alioupata kutokana na mazingira duni akija kupata watoto na wakati huo akiwa na mazingira mazuri basi tunategemea watoto wake waliokulia kwenye mazingira mazuri watakua warefu. Hata hivyo vinasaba vyote vya mwanadamu vilijulikana mwaka 2003 baada ya mpango wa kutafuta vinasaba vyote vya mwanadamu ulioitwa Human Genome Project kukamilika huko Marekani, lakini hakuna sehemu wameonesha kwenye vinasaba inayohusisha utofauti wa akili kati ya mataifa.

Nihitimishe kwa kusema kwamba akili huweza kubadilika kutokana na mazingira mtu aliyomo. Vilevile sisi waafrika tuache kujiona kwamba hatuna akili na tusimkuze sana mtu mweupe maana inawezekana kua kama yeye kiakili au kumpita. Tafiti zilizofanywa na Steele na Aronson mwaka 1995 zilionesha kwamba watu kuitwa na kukubali kua wao wana uwezo mdogo wa akili pia huwafanya kushindwa kufikiria barabara na kupata vizuri kwenye majaribio ya IQ. Kitu kikubwa kabisa kilichooneshwa na tafiti kwamba chaweza kukuza IQ ni elimu bora, vingine ni kama kukuza uwezo wa kukumbuka vitu na mazoezi hasa kwa wazee. Haihitaji mtu kuambiwa kuboresha elimu katika nchi kwa ujumla kutasababisha tuishi maisha ya kuridhisha zaidi kwa kutatua matatizo yetu.

8 comments:

  1. Umejitahidi sana kuweka mambo bayana,nimependa kazi hii, jamii ilikua imefumbwa....

    ReplyDelete
  2. Enter your comment...kila jamii inayojitegemea inauwezo wakiakili kulingana na mazingira yao,pia huwezo wakutatua matatizo unaligana na matatizo yaliopo katika jamii husika....kwa mfano ikitokea njaa,jamii husika itajifunza kutunza chakula
    achalia mbali na watu wenye uwezo watofauti katika jamii(genius minds) ambao wameweza kugundua vitu vya kipekee kama umeme,speed ya mwanga nk

    ReplyDelete
  3. Nice work Joseph Masalu

    ReplyDelete