Intaneti kwa upande mmoja imetusaidia kwa kiasi kikubwa sana
na siwezi kufikiria maisha yangekuwa vipi bila intaneti, ila kwa upande
mwingine intaneti imetulisha taarifa za uwongo zenye kutuletea madhara. Hii ni
kwa sababu kwenye ulimwengu wa intaneti mtu yoyote bila kujali kama ana weredi
wa fani fulani ama hana anaweza kuzungumzia kitu chochote na akasikilizwa.
Moja kati ya sehemu ambapo intaneti imefanya watu wavamie
fani za wengine na kujivisha kofia za ubobezi wakaanza kutoa elimu ni kwenye
fani ya afya. sisemi kwamba mtu mwingine haruhusiwi kutoa mawazo yake juu ya
mambo mbalimbali ya afya kwa jinsi anavyoona yeye, ila ninachosema ni kwamba
kuna watu wameingilia fani hii ya afya na kujifanya wao wanatoa
elimu(inayoambatana na kufanya biashara za matakataka yao) kiasi cha kupotosha
na kuumiza watu tena wasitumie hata tafiti kama wataalamu wa afya tunavyofanya
kwa kawaida. Labda niwaambie tu kwamba fani ya afya si kama ulivyo ulimwengu wa
kandanda ambamo kila shabiki anafikiri anaweza kuwa kocha wa timu pale
anapomkosoa kocha aliyepo.
Intaneti hutumika na wataalamu wa afya kupata na kusambaza elimu
kwa haraka na kwa urahisi zaidi, intaneti hiyohiyo hutumika na wanajamii
kujifunza juu ya hali zao kiafya. Lakini makundi haya mawili huchukua taarifa
kutoka sehemu mbili tofauti japo zote ni ndani ya intaneti. Mimi nikitaka
kujifunza juu ya swala fulani la afya, ninajua mahali pa kuzipata taarifa hizo
na mara nyingi huwa ni vyanzo vya kujifunzia ambamo sana sana tutaelewana watu
wa fani ya afya lakini tumejifunza kuzitafuna taarifa hizo na kuziweka katika
mfumo ambao mtu asiye mtaalamu anaweza kuelewa nae. Mwanajamii yeye anaweza
kujikuta anasoma taarifa ya aina yoyote ile bila kujua kama ni sahihi ama la!
Na kiuchuguzi changu kidogo nilichokifanya kwenye intaneti kwa kutafuta taarifa
za afya inaonesha uwezekano wa kukutana na taarifa zisizo sahihi ni mkubwa zaidi
ya zile zilizo sahihi kwani magugu ni mengi zaidi ya mazao.
Sio kila kitu unachokikuta kwenye intaneti ni sahihi. Bwana
mmoja kwenye tovuti iitwayo www.fadhilipaulo.com
anatuambia yeye anaijua sababu ya pumu ambayo ni kupungukiwa na maji mwilini tu
kama alivyofikiri mtu mmoja aliyejiita Dr. Batmanghelidj. Kwahiyo watu wenye
pumu wanywe tu maji na chumvi. Pia kwenye tovuti hiyo anatupa tiba mbadala
mbalimbali za pumu kama vile vitunguu swaumu, tangawizi, mafuta ya mharadali,
mtini, mafuta ya mkaratusi, asali, kitunguu maji, na vinginevyo, na mwisho
anaacha namba yake kama utahitaji dawa hizi za pumu basi umtafute akuuzie. Sasa
huyu mtu ametuambia pumu si ugonjwa bali ni upungufu tu wa maji mwilini halafu
ghafla anataka kutuuzia dawa zake za pumu(naomba aniache ninywe maji), hii
haiingii akilini japo ipo kwenye intaneti. Usipotoshwe na taarifa kama hizi
ukaacha ama ukamwachisha mwanao dawa kama una/ana pumu, pumu yaweza kuondoka na
uhai wa mtu. Mbali na hayo, utafiti uliofanywa na profesa wa kwanza wa tiba
mbadala aitwaye Edzard Ernst ulionesha kwamba hakuna tiba mbadala yenye uwezo
wa kutibu pumu. Kwenye hii tovuti pia watu wenye shinikizo la juu la damu
wanashauriwa kula zaidi chumvi na kunywa maji mengi, kinyume kabisa na ushauri
wa kitaalamu. Kwamba anashangaa kwanini ni muda mrefu sasa tumeambiwa kupunguza
kiasi cha chumvi tunayokula lakini tatizo la shinikizo la juu la damu
halijaisha? sijui nani aliyemwambia chumvi pekee ni sababu ya shinikizo la juu
la damu na ukiacha kuila basi hutopata hilo tatizo. Huyu hafahamu kwamba ni 5%
pekee ya shinikizo la juu la damu ndimo tunaweza kujua sababu ila kwenye 95%
hatujui sababu ila angalau tunajua tabia zinazoambatana na uwezekano mkubwa wa
mtu kupata shinikizo la juu la damu kama vile matumizi makubwa ya chumvi, kuwa
na ndugu wa karibu mwenye tatizo hilo, unene, kutokufanya mazoezi n.k. Tovuti
hii ukianza kuisoma wameiba maneno ya kisayansi na kuchanganya na mambo
wanayoyajua wenyewe na mwisho wa siku nia yao ni waonekane ni wataalamu na pili
waoneshe jinsi tiba ya kisasa isivyoweza na mwisho wauze bidhaa zao.
Mwingine ambaye anafanya kitu cha hatari zaidi na angepaswa
hata kufunguliwa mashtaka anamiliki blog inaitwa salimmsangi.Blogspot.com. Yeye
anawashauri wazazi wasipeleke watoto wao kupata chanjo kwani chanjo zina
madhara (bila kuyataja hayo madhara). Huyu ni wa kumpuuza kabisa kwani
inaonekana ameangalia hiki kitu kwenye mitandao ya nchi zilizoendelea ambako
watu wameanza kuyasahau magonjwa ya kuambukiza na wale wajinga wa kule
wasioweza kuzielewa vyema mbinu za kisayansi wanaosema kila mawazo yanatakiwa
yasikilizwe hata kama ni ya kijinga wanapiga harakati za kuzuia chanjo kwa
watoto. Chanjo ikiwafikia namba kadhaa ya watu kwenye jamii basi inakua
inatosha kuzuia maambukizi (wataalamu wanaita herd immunity), na mtu ambaye hajamchanja mwanae anapoona hapati
maambukizi huweza kujidanganya kuwa chanjo haina umuhimu. Tuwachanje watoto
wetu kwani na umasikini wetu huu hatutaweza kupambana na milipuko ya magonjwa
ambayo kinga tayari ipo.
Ninaposema Dokta Google namaanisha taarifa za kuhusu afya
unazozipata kwenye intaneti bila kujali zinatoka wapi. Kwa ushauri tu kuhusu dokta
google: penda kufuata ushauri wa daktari zaidi kuliko ule ambao unausoma kwenye
mitandao na kama kukitokea tofauti basi ni busara kumuuliza mtaalamu. Pia,
kusoma vitu kwenye mtandao na kulinganisha na alichokifanya daktari wako na
kuhitimisha kwamba hajui kwa sababu wewe umeangalia kwenye mtandao huenda
kukakugharimu wewe kwani ni bora kuuliza na kujadiliana kuliko kuhitimisha
hivyo. Ikitokea unapata taarifa za afya kutoka kwenye mitandao, runinga,
majarida ama magazeti basi ni vyema kujua yule anaetoa taarifa ile ana elimu
gani inayomfanya atoe taarifa ile ili basi hata akiwa ni mchungaji anatuambia
amemuombea mtu mwenye HIV na majibu yamekuja negative basi tutajua huenda kwake
negative ina maana nyingine. Na muda wote tukumbuke ni vyema na ni bora zaidi
kuanza na tiba za kisasa kabla ya tiba mbadala(si ndiyo maana zikaitwa mbadala
jamani), miguu ikivimba usianze kujipaka mikaa miguuni bali nenda kwanza
hospitali. Mwisho nikazie tu kwamba sio kila taarifa ya kwenye inataneti ni
sahihi.
Hili jambo limeikumba si tu jamii yetu ya Tanzania bali hata wenzetu wa nchi zikizoendelea, hii inatokana na utafiti uliofanywa na wanasanyansi nchini marekani ambao ulilenga tovuti mbalimbali haya ile maarufu ya Wikipedia. Utafiti huo ulionesha kuwa kati ya mambo kumi yaliyoandikwa katika tovuti hiyo ya Wikipedia kuhusu afya tisa kati yao yalikuwa na makosa mengi. Hivyo basi ni jambo la msingi sana kuzungumza na daktari wako na sio Wikipedia.
ReplyDeleteInternet ina mazuri yote na upuuzi wote😀
DeleteUmesema yote ,sina la kusema ,kazi nzur
ReplyDeleteTupo pamoja mkuu
Delete