Saturday, 22 October 2016

DOKTA GOOGLE



Intaneti kwa upande mmoja imetusaidia kwa kiasi kikubwa sana na siwezi kufikiria maisha yangekuwa vipi bila intaneti, ila kwa upande mwingine intaneti imetulisha taarifa za uwongo zenye kutuletea madhara. Hii ni kwa sababu kwenye ulimwengu wa intaneti mtu yoyote bila kujali kama ana weredi wa fani fulani ama hana anaweza kuzungumzia kitu chochote na akasikilizwa.
 Image result for doctor google
Moja kati ya sehemu ambapo intaneti imefanya watu wavamie fani za wengine na kujivisha kofia za ubobezi wakaanza kutoa elimu ni kwenye fani ya afya. sisemi kwamba mtu mwingine haruhusiwi kutoa mawazo yake juu ya mambo mbalimbali ya afya kwa jinsi anavyoona yeye, ila ninachosema ni kwamba kuna watu wameingilia fani hii ya afya na kujifanya wao wanatoa elimu(inayoambatana na kufanya biashara za matakataka yao) kiasi cha kupotosha na kuumiza watu tena wasitumie hata tafiti kama wataalamu wa afya tunavyofanya kwa kawaida. Labda niwaambie tu kwamba fani ya afya si kama ulivyo ulimwengu wa kandanda ambamo kila shabiki anafikiri anaweza kuwa kocha wa timu pale anapomkosoa kocha aliyepo.

Intaneti hutumika na wataalamu wa afya kupata na kusambaza elimu kwa haraka na kwa urahisi zaidi, intaneti hiyohiyo hutumika na wanajamii kujifunza juu ya hali zao kiafya. Lakini makundi haya mawili huchukua taarifa kutoka sehemu mbili tofauti japo zote ni ndani ya intaneti. Mimi nikitaka kujifunza juu ya swala fulani la afya, ninajua mahali pa kuzipata taarifa hizo na mara nyingi huwa ni vyanzo vya kujifunzia ambamo sana sana tutaelewana watu wa fani ya afya lakini tumejifunza kuzitafuna taarifa hizo na kuziweka katika mfumo ambao mtu asiye mtaalamu anaweza kuelewa nae. Mwanajamii yeye anaweza kujikuta anasoma taarifa ya aina yoyote ile bila kujua kama ni sahihi ama la! Na kiuchuguzi changu kidogo nilichokifanya kwenye intaneti kwa kutafuta taarifa za afya inaonesha uwezekano wa kukutana na taarifa zisizo sahihi ni mkubwa zaidi ya zile zilizo sahihi kwani magugu ni mengi zaidi ya mazao.

Sio kila kitu unachokikuta kwenye intaneti ni sahihi. Bwana mmoja kwenye tovuti iitwayo www.fadhilipaulo.com anatuambia yeye anaijua sababu ya pumu ambayo ni kupungukiwa na maji mwilini tu kama alivyofikiri mtu mmoja aliyejiita Dr. Batmanghelidj. Kwahiyo watu wenye pumu wanywe tu maji na chumvi. Pia kwenye tovuti hiyo anatupa tiba mbadala mbalimbali za pumu kama vile vitunguu swaumu, tangawizi, mafuta ya mharadali, mtini, mafuta ya mkaratusi, asali, kitunguu maji, na vinginevyo, na mwisho anaacha namba yake kama utahitaji dawa hizi za pumu basi umtafute akuuzie. Sasa huyu mtu ametuambia pumu si ugonjwa bali ni upungufu tu wa maji mwilini halafu ghafla anataka kutuuzia dawa zake za pumu(naomba aniache ninywe maji), hii haiingii akilini japo ipo kwenye intaneti. Usipotoshwe na taarifa kama hizi ukaacha ama ukamwachisha mwanao dawa kama una/ana pumu, pumu yaweza kuondoka na uhai wa mtu. Mbali na hayo, utafiti uliofanywa na profesa wa kwanza wa tiba mbadala aitwaye Edzard Ernst ulionesha kwamba hakuna tiba mbadala yenye uwezo wa kutibu pumu. Kwenye hii tovuti pia watu wenye shinikizo la juu la damu wanashauriwa kula zaidi chumvi na kunywa maji mengi, kinyume kabisa na ushauri wa kitaalamu. Kwamba anashangaa kwanini ni muda mrefu sasa tumeambiwa kupunguza kiasi cha chumvi tunayokula lakini tatizo la shinikizo la juu la damu halijaisha? sijui nani aliyemwambia chumvi pekee ni sababu ya shinikizo la juu la damu na ukiacha kuila basi hutopata hilo tatizo. Huyu hafahamu kwamba ni 5% pekee ya shinikizo la juu la damu ndimo tunaweza kujua sababu ila kwenye 95% hatujui sababu ila angalau tunajua tabia zinazoambatana na uwezekano mkubwa wa mtu kupata shinikizo la juu la damu kama vile matumizi makubwa ya chumvi, kuwa na ndugu wa karibu mwenye tatizo hilo, unene, kutokufanya mazoezi n.k. Tovuti hii ukianza kuisoma wameiba maneno ya kisayansi na kuchanganya na mambo wanayoyajua wenyewe na mwisho wa siku nia yao ni waonekane ni wataalamu na pili waoneshe jinsi tiba ya kisasa isivyoweza na mwisho wauze bidhaa zao.

Mwingine ambaye anafanya kitu cha hatari zaidi na angepaswa hata kufunguliwa mashtaka anamiliki blog inaitwa salimmsangi.Blogspot.com. Yeye anawashauri wazazi wasipeleke watoto wao kupata chanjo kwani chanjo zina madhara (bila kuyataja hayo madhara). Huyu ni wa kumpuuza kabisa kwani inaonekana ameangalia hiki kitu kwenye mitandao ya nchi zilizoendelea ambako watu wameanza kuyasahau magonjwa ya kuambukiza na wale wajinga wa kule wasioweza kuzielewa vyema mbinu za kisayansi wanaosema kila mawazo yanatakiwa yasikilizwe hata kama ni ya kijinga wanapiga harakati za kuzuia chanjo kwa watoto. Chanjo ikiwafikia namba kadhaa ya watu kwenye jamii basi inakua inatosha kuzuia maambukizi (wataalamu wanaita herd immunity), na mtu ambaye hajamchanja mwanae anapoona hapati maambukizi huweza kujidanganya kuwa chanjo haina umuhimu. Tuwachanje watoto wetu kwani na umasikini wetu huu hatutaweza kupambana na milipuko ya magonjwa ambayo kinga tayari ipo.

Ninaposema Dokta Google namaanisha taarifa za kuhusu afya unazozipata kwenye intaneti bila kujali zinatoka wapi. Kwa ushauri tu kuhusu dokta google: penda kufuata ushauri wa daktari zaidi kuliko ule ambao unausoma kwenye mitandao na kama kukitokea tofauti basi ni busara kumuuliza mtaalamu. Pia, kusoma vitu kwenye mtandao na kulinganisha na alichokifanya daktari wako na kuhitimisha kwamba hajui kwa sababu wewe umeangalia kwenye mtandao huenda kukakugharimu wewe kwani ni bora kuuliza na kujadiliana kuliko kuhitimisha hivyo. Ikitokea unapata taarifa za afya kutoka kwenye mitandao, runinga, majarida ama magazeti basi ni vyema kujua yule anaetoa taarifa ile ana elimu gani inayomfanya atoe taarifa ile ili basi hata akiwa ni mchungaji anatuambia amemuombea mtu mwenye HIV na majibu yamekuja negative basi tutajua huenda kwake negative ina maana nyingine. Na muda wote tukumbuke ni vyema na ni bora zaidi kuanza na tiba za kisasa kabla ya tiba mbadala(si ndiyo maana zikaitwa mbadala jamani), miguu ikivimba usianze kujipaka mikaa miguuni bali nenda kwanza hospitali. Mwisho nikazie tu kwamba sio kila taarifa ya kwenye inataneti ni sahihi.

4 comments:

  1. Hili jambo limeikumba si tu jamii yetu ya Tanzania bali hata wenzetu wa nchi zikizoendelea, hii inatokana na utafiti uliofanywa na wanasanyansi nchini marekani ambao ulilenga tovuti mbalimbali haya ile maarufu ya Wikipedia. Utafiti huo ulionesha kuwa kati ya mambo kumi yaliyoandikwa katika tovuti hiyo ya Wikipedia kuhusu afya tisa kati yao yalikuwa na makosa mengi. Hivyo basi ni jambo la msingi sana kuzungumza na daktari wako na sio Wikipedia.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Internet ina mazuri yote na upuuzi wote😀

      Delete
  2. Umesema yote ,sina la kusema ,kazi nzur

    ReplyDelete