Saturday, 26 November 2016

MAOMBI KAMA TIBA



Binafsi nikisikia neno maombi kumbukumbu inayokuja kichwani huwa si ya kupendeza kabisa. Mnamo mwaka 2002 nilishuhudia mtoto mdogo anagongwa na gali. Inaonekana alikuwa na mama yake na walikuwa wamekuja eneo lile kwa ajili ya huduma za kiroho maana ilikuwa ni barabara ya kuvuka kutokea kanisani. Baada ya kumgonga gali lile lilikimbia na watu waliokuwa eneo lile wengi walikuwa wamekuja kanisani pia. Walimuokota yule mtoto aliyekuwa amepoteza fahamu na kisha kumpeleka kanisani kwa ajili ya kuombewa ili aponywe. Nilichosikia kesho yake ni kwamba yule mtoto alifariki. Baada ya kujifunza mambo ya afya na uponyaji (kwa tiba za kisasa lakini) miaka mingi baadae, sijaacha kuhisi nini kilimfanya mtoto yule kufariki na kama matokeo yangebadilika iwapo angewahishwa hospitalini. Mfano, baada ya kupoteza fahamu mtoto yule labda alizibwa hewa na ulimi wake; mchungaji sidhani kama angeweza kumfungua mdomo ili auweke vizuri ulimi wake. Ama labda hata kama angepelekwa hospitali hakuna ambalo lingebadilika, sina uhakika ila ninachoamini ni kwamba wangefanya kitu cha msingi Zaidi ya mchungaji. Huu ni mfano hasi ila pia ninao mfano chanya: mmoja kati ya mama zangu wadogo aliwahi kuwa anasumbuliwa sana na madonda ya tumbo kwa muda mrefu. Anasema alitumia dawa ila hakupata nafuu. Siku moja akiwa amelala aliamka usiku wa manane kutokana na maumivu ya tumbo na kwenye redio alimsikia mchungaji anahubiri na akasema kama kuna sehemu inauma uishike na itapona; basi alishika tumbo  na tangu siku hiyo yeye amepona madonda ya tumbo.
Image result for mchungaji dawa ya mbu
Huenda wengi hatufahamu ila maombi yakitumika kama tiba basi hiyo nayo ni tiba mbadala kwani maana ya tiba mbadala ni tiba zote ambazo hazipo kwenye tiba za kisasa, tiba za kisayansi, tiba za magharibi. Tiba ya maombi hutumia “nguvu” inayotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ambae ndiye mgonjwa na kumponya. Neno nguvu kama linavyotumika hapa sio katika ile maana ya nguvu kama ile nguvu ya umeme kusukuma mashine ila ni nguvu ikiwa  na maana ya kiroho, nguvu ambayo sisi hatuwezi kuiona ila wanasema ipo.

Ni kweli maombi yana uwezo wa kuponya kupitia iyo nguvu? Ama kuna namna ya kuyaelezea mambo? Tafiti zilizofanywa kuliangalia hili zimeonesha kwamba hakuna nguvu iliyopo bali kilichopo ni kwamba maombi yana placebo kubwa sana (huko nyuma nimewahi kuelezea maana ya placebo). Wagonjwa wakiwa wanaombewa na wanafahamu kuwa wanaombewa basi wanapata faraja na kuhisi upendo, hiyo huweza kuharakisha uponaji wao ila pia huweza kuwafanya wajisikie vizuri na kuhisi kupona hata kama bado wana ugonjwa. Wagonjwa wanaoombewa ila hawajui kama wanaombewa hawapati mabadiliko yoyote yale yanayotokana na maombi yale. Huko USA mwaka 2006 yalichapishwa matokeo ya tafiti iliyofanywa kwa miaka 10 na kugharimu dola za kimarekani milioni 2.5. Utafiti huo ulihusisha wagonjwa 10,000 waliokuwa wamefanyiwa opasuaji wa mishipa ya moyo kwenye hospitali sita za nchi hiyo ikiwemo Havard. Wagonjwa hao waligawiwa kwenye makundi mawili na kundi moja likaombewa kwa miaka yote iyo kumi ila kundi jingine halikuombewa. Hakuna mgonjwa aliyejua kundi alimo. Mwisho wa siku ilionekana makundi yote mawili yalikuwa na maendeleo sawa tu na hakukuwa na tofauti iliyoletwa na maombi. Imani ya watu juu ya maombi ndiyo ishu hapa na sio nguvu ya waponyaji.

Kila tukifungua runinga zetu tunawaona watu wengi ambao wanatoa ushuhuda juu ya kuponywa kwao na wachungaji wanaomiliki kanisa na kipindi kinachooneshwa. Wengine hata wanasema walikuwa na magonjwa makubwa kama saratani ama maambukizi ya VVU na wameponywa. Hawa huwa tunawaona mara moja tu na hatuwafatilii wanakwenda wapi baadae, kama kweli walikuwa na magonjwa makubwa kama haya na wakaamini wameponywa na maombi na wakaachana na tiba nyingine basi tukiwatafuta miaka ya baadae tutakutana na vyeti vyao vya kifo tu. Mtu akisema ana saratani swali la kwanza lapaswa kuwa amejuaje na kama hajafanya vipimo mfano kutoa kinyama kilichopelekwa kuchunguzwa basi huyo ni muongo tu. Wachungaji wengine wameenda mbali na wanadai wanaweza kufufua hata watu waliokufa. Japo sijawahi kusikia hao waliokufa nani aliwathibitisha kwamba wamekufa, na sijaona mtu akiwahoji walipokufa walienda wapi. Ila hata kama wakithibitishwa, anaewathibitisha ni mwanadamu pia. Yule mtoto wa panya road aliezinduka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Temeke akizaniwa amefariki ni mfano tosha, kama ingetokea mchungaji amemuombea kabla basi angechukua sifa za kufufua zisizomstahili. Ila wenye uwezo wa kufufua watu, tuwashauri watembelee vyumba vya maiti mahospitalini kwani huko ndiko waliko wengi waliofariki.

Mtu hakatazwi kuombewa ila maombi hayapaswi kuchukua nafasi ya tiba kwani kuna matatizo mengi yatatokea. Waombeaji pia baada ya kuombea hawatoi hata njia za kujizuia na magonjwa mfano kulala kwenye neti, kunawa mikono, ngono salama, kufanya mazoezi na kadhalika, wao wanasubiri tu uumwe ndio watoe huduma. Pia tukumbuke maombi yamekuwepo tangu kitambo sana, tangu enzi za Yesu ila tiba za kweli zimetokea ndani ya miaka 100 tu iliyopita kutokana na kukua kwa sayansi. Mfano zamani ukiwa na kifua kikuu basi una wigo mfinyu sana wa kuishi na maombi yalikuwepo, ila kwa sasa kuna dawa na utapona.

3 comments:

  1. Nakuelewa sana Daktari Masalu, Madini muhimu kwa jamii, maarifa yanabadilisha mtazamo ya watu , endelea kutoa maarifa kwa mambo haya ambayo jamii yetu imekuwa na uelewa wa upande mmoja tuu......... Sayansi ndio njia muafaka ya kujibu maswali magumu yanayohusu maisha yetu ya kila siku...... Miaka ya nyuma ilikuwa ukiwa na Malaria kali (Cerebral Malaria) watu walikuwa wanasema unamapepo na wanakazana kukuombea lakini siku hizi tunakukaza Quinine na unapona..... Napenda sana Sayansi aiseee.... #HongeraDrJosephMasalu

    ReplyDelete