Binafsi nikisikia neno maombi kumbukumbu inayokuja kichwani
huwa si ya kupendeza kabisa. Mnamo mwaka 2002 nilishuhudia mtoto mdogo
anagongwa na gali. Inaonekana alikuwa na mama yake na walikuwa wamekuja eneo
lile kwa ajili ya huduma za kiroho maana ilikuwa ni barabara ya kuvuka kutokea
kanisani. Baada ya kumgonga gali lile lilikimbia na watu waliokuwa eneo lile
wengi walikuwa wamekuja kanisani pia. Walimuokota yule mtoto aliyekuwa
amepoteza fahamu na kisha kumpeleka kanisani kwa ajili ya kuombewa ili aponywe.
Nilichosikia kesho yake ni kwamba yule mtoto alifariki. Baada ya kujifunza
mambo ya afya na uponyaji (kwa tiba za kisasa lakini) miaka mingi baadae,
sijaacha kuhisi nini kilimfanya mtoto yule kufariki na kama matokeo
yangebadilika iwapo angewahishwa hospitalini. Mfano, baada ya kupoteza fahamu
mtoto yule labda alizibwa hewa na ulimi wake; mchungaji sidhani kama angeweza
kumfungua mdomo ili auweke vizuri ulimi wake. Ama labda hata kama angepelekwa
hospitali hakuna ambalo lingebadilika, sina uhakika ila ninachoamini ni kwamba
wangefanya kitu cha msingi Zaidi ya mchungaji. Huu ni mfano hasi ila pia ninao
mfano chanya: mmoja kati ya mama zangu wadogo aliwahi kuwa anasumbuliwa sana na
madonda ya tumbo kwa muda mrefu. Anasema alitumia dawa ila hakupata nafuu. Siku
moja akiwa amelala aliamka usiku wa manane kutokana na maumivu ya tumbo na
kwenye redio alimsikia mchungaji anahubiri na akasema kama kuna sehemu inauma
uishike na itapona; basi alishika tumbo
na tangu siku hiyo yeye amepona madonda ya tumbo.

Huenda wengi hatufahamu ila maombi yakitumika kama tiba basi
hiyo nayo ni tiba mbadala kwani maana ya tiba mbadala ni tiba zote ambazo
hazipo kwenye tiba za kisasa, tiba za kisayansi, tiba za magharibi. Tiba ya
maombi hutumia “nguvu” inayotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ambae ndiye
mgonjwa na kumponya. Neno nguvu kama linavyotumika hapa sio katika ile maana ya
nguvu kama ile nguvu ya umeme kusukuma mashine ila ni nguvu ikiwa na maana ya kiroho, nguvu ambayo sisi
hatuwezi kuiona ila wanasema ipo.
Ni kweli maombi yana uwezo wa kuponya kupitia iyo nguvu? Ama
kuna namna ya kuyaelezea mambo? Tafiti zilizofanywa kuliangalia hili zimeonesha
kwamba hakuna nguvu iliyopo bali kilichopo ni kwamba maombi yana placebo kubwa
sana (huko nyuma nimewahi kuelezea maana ya placebo). Wagonjwa wakiwa
wanaombewa na wanafahamu kuwa wanaombewa basi wanapata faraja na kuhisi upendo,
hiyo huweza kuharakisha uponaji wao ila pia huweza kuwafanya wajisikie vizuri
na kuhisi kupona hata kama bado wana ugonjwa. Wagonjwa wanaoombewa ila hawajui kama
wanaombewa hawapati mabadiliko yoyote yale yanayotokana na maombi yale. Huko
USA mwaka 2006 yalichapishwa matokeo ya tafiti iliyofanywa kwa miaka 10 na
kugharimu dola za kimarekani milioni 2.5. Utafiti huo ulihusisha wagonjwa
10,000 waliokuwa wamefanyiwa opasuaji wa mishipa ya moyo kwenye hospitali sita
za nchi hiyo ikiwemo Havard. Wagonjwa hao waligawiwa kwenye makundi mawili na
kundi moja likaombewa kwa miaka yote iyo kumi ila kundi jingine halikuombewa.
Hakuna mgonjwa aliyejua kundi alimo. Mwisho wa siku ilionekana makundi yote
mawili yalikuwa na maendeleo sawa tu na hakukuwa na tofauti iliyoletwa na
maombi. Imani ya watu juu ya maombi ndiyo ishu hapa na sio nguvu ya waponyaji.
Kila tukifungua runinga zetu tunawaona watu wengi ambao
wanatoa ushuhuda juu ya kuponywa kwao na wachungaji wanaomiliki kanisa na
kipindi kinachooneshwa. Wengine hata wanasema walikuwa na magonjwa makubwa kama
saratani ama maambukizi ya VVU na wameponywa. Hawa huwa tunawaona mara moja tu
na hatuwafatilii wanakwenda wapi baadae, kama kweli walikuwa na magonjwa makubwa
kama haya na wakaamini wameponywa na maombi na wakaachana na tiba nyingine basi
tukiwatafuta miaka ya baadae tutakutana na vyeti vyao vya kifo tu. Mtu akisema
ana saratani swali la kwanza lapaswa kuwa amejuaje na kama hajafanya vipimo
mfano kutoa kinyama kilichopelekwa kuchunguzwa basi huyo ni muongo tu. Wachungaji
wengine wameenda mbali na wanadai wanaweza kufufua hata watu waliokufa. Japo
sijawahi kusikia hao waliokufa nani aliwathibitisha kwamba wamekufa, na sijaona
mtu akiwahoji walipokufa walienda wapi. Ila hata kama wakithibitishwa,
anaewathibitisha ni mwanadamu pia. Yule mtoto wa panya road aliezinduka kwenye
chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Temeke akizaniwa amefariki ni
mfano tosha, kama ingetokea mchungaji amemuombea kabla basi angechukua sifa za
kufufua zisizomstahili. Ila wenye uwezo wa kufufua watu, tuwashauri watembelee
vyumba vya maiti mahospitalini kwani huko ndiko waliko wengi waliofariki.
Mtu hakatazwi kuombewa ila maombi hayapaswi kuchukua nafasi
ya tiba kwani kuna matatizo mengi yatatokea. Waombeaji pia baada ya kuombea
hawatoi hata njia za kujizuia na magonjwa mfano kulala kwenye neti, kunawa
mikono, ngono salama, kufanya mazoezi na kadhalika, wao wanasubiri tu uumwe
ndio watoe huduma. Pia tukumbuke maombi yamekuwepo tangu kitambo sana, tangu
enzi za Yesu ila tiba za kweli zimetokea ndani ya miaka 100 tu iliyopita
kutokana na kukua kwa sayansi. Mfano zamani ukiwa na kifua kikuu basi una wigo
mfinyu sana wa kuishi na maombi yalikuwepo, ila kwa sasa kuna dawa na utapona.
Nakuelewa sana Daktari Masalu, Madini muhimu kwa jamii, maarifa yanabadilisha mtazamo ya watu , endelea kutoa maarifa kwa mambo haya ambayo jamii yetu imekuwa na uelewa wa upande mmoja tuu......... Sayansi ndio njia muafaka ya kujibu maswali magumu yanayohusu maisha yetu ya kila siku...... Miaka ya nyuma ilikuwa ukiwa na Malaria kali (Cerebral Malaria) watu walikuwa wanasema unamapepo na wanakazana kukuombea lakini siku hizi tunakukaza Quinine na unapona..... Napenda sana Sayansi aiseee.... #HongeraDrJosephMasalu
ReplyDeletePamoja sana mkuu
DeleteKazi nzuri sana
Delete